Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANA NA WADAU KUJADILI NAULI ZA MV NEW MWANZA

Imewekwa: 16 December, 2025
TASAC YAKUTANA NA WADAU KUJADILI NAULI ZA MV NEW MWANZA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 15 Desemba, 2025, limekutana na wadau wa sekta ya usafiri majini, jijini Mwanza kwa ajili ya kupokea na kujadili maombi ya Shirika la Meli Tanzania (TASHICO), kuhusu tozo za nauli za abiria na mizigo kwa meli ya MV New Mwanza inayofanya safari kati Mwanza na Bukoba. 

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla ambaye alikua mwenyekiti wa kikao hicho ameeleza kuwa zoezi la ushirikishwaji wa wadau ni muhimu ili kuhakikisha kuwa tozo zitakazoidhinishwa zinazingatia maslahi ya watumiaji wa huduma na kwamba zinaendana na gharama halisi za uendeshaji. 

Bw. Sigalla amesema kuwa kikao hicho kinafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415, kinachoitaka TASAC kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufanya uamuzi wowote wa kupitisha tozo au viwango vya huduma. 

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Patrick Karangwa ameipongeza TASAC kwa kufanya kikao hicho na kupongeza ushiriki wa wadau wengi kutoka sekta binafsi.

Akiwasilisha wasilisho kuhusu viwango vinavyopendekezwa, Afisa Uendeshaji TASHICO, Bw. Prosper Rwelengera amesema kuwa meli ya MV New Mwanza, ina uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo pamoja na magari, na inatarajiwa kuchukua takribani saa sita kusafiri kutoka Mwanza hadi Bukoba. 

Kwa upande wao, wadau waliipongeza Serikali kwa kukamilisha mradi wa meli hiyo pamoja na mchango wake katika kuchochea biashara na usafiri salama kati ya Mwanza na Bukoba. Waliongeza kuwa kuna umuhimu wa kulinda ubora na uhakika wa huduma sambamba na tozo zitakazoidhinishwa.

Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa uwazi na ushirikishwaji wa TASAC unaolenga kulinda maslahi ya umma, kuhakikisha uendelevu wa huduma za usafiri kwa njia ya maji hapa nchini

Mrejesho, Malalamiko au Wazo