TASAC YAKUTANA NA MAWAKALA WA MELI KUJADILI CHANGAMOTO YA MAKASHA TUPU
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 8 Mei 2026, limekutana na mawakala wa meli jijini Dar es Salaam kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji wa kushusha makasha tupu katika bandari kavu, hali inayochangia msongamano na kuathiri ufanisi wa mnyororo wa usafirishaji nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Meneja Udhibiti wa Huduma ya Usafiri Meli wa TASAC, Bi. Fatuma Masenene, alisema kikao hicho kililenga kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto zinazotokana na ongezeko la makasha tupu pamoja na kuhakikisha huduma za bandari zinaendelea kuwa bora na zenye ufanisi.
Alisema baadhi ya makasha tupu yamekuwa yakikaa kwa muda mrefu kwenye malori bila kushushwa katika maeneo yaliyopangwa, hali inayosababisha msongamano katika bandari kavu na kuathiri mtiririko wa shughuli za usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya Bandari ya Dar es Salaam.
Bi. Masenene alisisitiza kuwa TASAC inaendelea kusimamia kwa karibu uratibu wa huduma za usafirishaji na shughuli za mawakala wa meli ili kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri wa majini na usafirishaji kwa ujumla.
Kwa upande wao, mawakala wa meli na wadau wengine walieleza changamoto zinazochangia kuchelewa kwa ushushaji wa makasha tupu, ikiwemo msongamano wa magari barabarani, muda mrefu wa kusafirisha makasha bandarini pamoja na changamoto za miundombinu kutokana na ongezeko kubwa la magari yanayobeba makasha hayo.
Kikao hicho kilifikia makubaliano ya kuweka mikakati mbalimbali ya kuboresha hali hiyo, ikiwemo kuhakikisha makasha tupu yanapakiwa kwa asilimia 100 kulingana na mipango ya mawakala wa meli, kuruhusu matumizi ya baadhi ya barabara maalum nyakati za usiku kwa usafirishaji wa makasha tupu, pamoja na kutumia bandari kavu ya Kwala kuhifadhi makasha hayo kabla ya kusafirishwa kwa njia ya treni kuelekea bandarini.
TASAC imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji kuhakikisha changamoto zote zinazotokana na ongezeko la mizigo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa lengo la kuimarisha ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ubora wa huduma kwa taifa na nchi jirani zinazotumia bandari hiyo.