Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANA NA HALMASHAURI ZA JIJI LA DAR ES SALAAM NA TAASISI ZA SERIKALI KUJADILI USIMAMIZI WA BANDARI KAVU

Imewekwa: 08 May, 2026
TASAC YAKUTANA NA HALMASHAURI ZA JIJI LA DAR ES SALAAM NA TAASISI ZA SERIKALI KUJADILI USIMAMIZI WA BANDARI KAVU

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 8 Mei 2026, limefanya kikao maalum na maafisa kutoka Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena zinazopita katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kukua kwa biashara ya kikanda na kimataifa pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za usafirishaji ndani na nje ya nchi.

Amesema kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, Bandari ya Dar es Salaam inapokea zaidi ya makontena 110,000 kwa mwezi, huku uwezo wa eneo la ndani la bandari kuhifadhi makontena ukiwa takribani 27,000 na uwezo wa bandari kavu ukiwa makontena 35,000 kwa wakati mmoja katika kiwango cha juu cha matumizi, hali inayoonyesha mahitaji makubwa ya maeneo ya uhifadhi wa mizigo.

Bw. Salum ameeleza kuwa kwa ufanisi wa kitaalam, bandari inapaswa kuhudumia makontena kwa asilimia 65 ya uwezo wake ili kuruhusu shughuli nyingine za kibandari kuendelea bila usumbufu. Ameongeza kuwa kati ya makontena yote yanayoingia bandarini kila mwezi, asilimia 50 husafirishwa kwenda nchi jirani na asilimia nyingine 50 hubaki nchini. Kati ya mizigo inayobaki nchini, asilimia 90 hubaki katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na asilimia 10 husafirishwa kwenda mikoa mingine.

Aidha, amesema mizigo inayokwenda nje ya nchi kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ni zaidi ya makontena 46,000 kwa mwezi, hali inayoongeza umuhimu wa matumizi sahihi ya bandari kavu ili kupunguza msongamano bandarini na kuongeza ufanisi wa huduma.

Katika kikao hicho, wadau wamejadili mikakati ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji, matumizi bora ya bandari kavu na kuimarisha mtiririko wa biashara kati ya Tanzania na nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es Salaam.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo