Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKABIDHIWA BOTI YA DORIA KUPAMBANA NA UHALIFU MAJINI

Imewekwa: 20 September, 2024
TASAC YAKABIDHIWA BOTI YA DORIA KUPAMBANA NA UHALIFU MAJINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekabidhiwa boti ya doria ambayo imetolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni juhudi za Serikali katika kuimarisha shughuli za usimamizi na usalama wa bahari, hafla ya makabidhiano haya imefanyika katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam, leo, tarehe 19 Septemba, 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi amesema lengo kuu la kununuliwa kwa boti hiyo ni kuimarisha doria ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu nchini.

Amesema doria hizo ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vile uvuvi haramu, uhamiaji haramu, usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara za magendo na utoroshwaji wa nyara za Serikali.

"Boti hii imenunuliwa kupitia Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu Nchini kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Nitumie nafasi kuwashukuru wafadhili wetu hao kwa ufadhili huu na ushirikiano mkubwa waliotupatia wakati wote wa ununuzi wa boti hii," amesema Dkt. Yonazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kulipatia Shirika hilo boti hiyo na kusema kuwa itaongeza tija katika kupambana na uhalifu wa baharini na ulinzi wa rasilimali za bahari.

"Sisi kama Shirika, tutahakikisha boti hii inatunzwa vyema kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola nchini ili kutimiza malengo ya kununuliwa kwa boti hii ikiwemo ulinzi wa bahari, maziwa makuu pamoja na rasilimali zake," amesema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Naho. Mussa Mandia pamoja na wadau kutoka taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo