TASAC YAKABIDHI VIFAA TIBA SUMBAWANGA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 28 Januari, 2025, limekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni kumi 10 katika vituo vitatu vya afya vya Mtowisa, Nankanga na Milepa vilivyopo wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Msaada huo umetolewa kufuatia uhitaji wa vifaa hivyo mara baada ya kutokea kwa dhoruba ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, Ofisa Mwandamizi wa TASAC, Nah. David Chiragi amesema lengo la msaada huo ni kuhakikisha wanapunguza upungufu wa vifaa tiba katika vituo hivyo.
“Tumetoa msaada huu baada ya tukio la wavuvi 550 kukumbwa na adha ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa uliosababisha watu 10 kufa maji ambapo tisa waliopolewa na mmoja hakuweza kupatikana,” amesema Nah. Chiragi.
Aidha amesema kuwa moja ya jukumu la TASAC ni kusimamia masuala ya usalama ulinzi na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za vyombo vya usafiri majini.
Ameongeza kuwa TASAC wanaishukuru Serikali kwa kuonesha umoja na mshikamano na kuhakikisha zoezi la uokoaji linafanikiwa kwa kuokoa wavuvi 540 waliokumbwa na adha hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Chirugile akipokea msaada huo wa vifaa tiba katika zahanati ya kijiji cha Nankanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ameishukuru TASAC pamoja na Wizara ya Uchukuzi kwa msaada huo muhimu kwa Bonde la Ziwa Rukwa ambao utapunguza adha kwa wagonjwa na akina mama wajawazito kutokana na upungufu wa vifaa tiba katika vituo vya afya.
Msimamizi wa kituo cha kata ya Nankanga Elladonna Mpumpa alishukuru TASAC na Serikali kwa ukombozi mkubwa ambapo amesema wamekuwa na upungufu wa vifaa tiba.
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Nankanga wilaya ya Sumbawanga, Bw. Morice Fwaka kwa niaba ya wananchi aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada wa vifaa tiba ambapo msaada huo utakwenda kupunguza adha ya wagonjwa kulala wawili katika kitanda kimoja hasa akina mama wajawazito.