TASAC YAJIPANGA KUTUMIA UZOEFU WA NIMASA KUIMARISHA USIMAMIZI WA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepanga kutumia uzoefu kutoka kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Usalama ya Nigeria (NIMASA), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kujifunza mbinu bora za usimamizi wa sekta ya usafiri majini kwa maendeleo endelevu ya uchumi.
Lengo hilo limewekwa na ujumbe wa TASAC, uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Bi. Rukia Shamte ambaye ameambatana na baadhi ya wajumbe wa bodi na menejimenti ya TASAC wakati wa ziara ya siku nne ya mafunzo ya kimkakati katika makao makuu ya NIMASA, jijini Lagos, Nigeria.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Udhibiti, Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira, Bi. Leticia Mutaki amesema kuwa NIMASA ni taasisi ya mfano barani Afrika, na TASAC imekwenda kujifunza na kupata uzoefu wa mbinu bora zinazotumiwa nchini Nigeria.
"Ziara hii ni muhimu sana kwa TASAC kwani inalenga kuongeza uwezo wa kitaasisi na kuboresha mifumo yetu ya udhibiti. Kupitia ziara hii, tumepata maarifa yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi, na kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu nchini Tanzania," amesema Bi. Mutaki.
Wakiwa katika ziara hiyo, ujumbe wa TASAC ulipata fursa ya kujifunza kwa kina kuhusu mifumo ya usimamizi wa usalama wa meli, mikakati ya kukabiliana na uchafuzi wa bahari, matumizi ya teknolojia katika ufuatiliaji wa shughuli za baharini, pamoja na namna NIMASA inavyotekeleza majukumu yake ya kimataifa.
Mojawapo ya matokeo yanayotarajiwa ya ziara hii ni kutiwa saini kwa Mkataba wa Makubaliano (MoU) kati ya TASAC na NIMASA ambao utaweka misingi ya ushirikiano rasmi na wa kudumu katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya usafiri majini.