TASAC YAJIDHATITI KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA KWA MABAHARIA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), tarehe 20 Novemba, 2024, limefanya mazungumzo na kampuni ya uwakala wa kutafutia ajira mabaharia wa ijulikanayo kama CSCS International Manning ya Nchini Mauritius.
Kwa upande wa TASAC iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira, Bi. Leticia Mutaki na Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, Bw. Hamid Mbegu na kwa upande wa CSCS International Manning iliwakilishwa na Bw. Chandra Kumar Seepal Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo aliyeambatana na Bw. Riziki Maisara, Mtanzania aliyepata fursa ya ajira katika Kampuni hiyo.
Katika kikao hiko, wawakilishi hao walijadiliana jinsi ya kufungua fursa za ajira za mabaharia wa Tanzania kupitia kampuni hiyo ambayo inafanya kazi kwa karibu na kampuni kubwa ya meli ya kitalii ya Royal Caribbean.
Kwa mujibu wa Bw. Seepal, Kampuni ya CSCS International Manning ina fursa lukuki ambazo mabaharia wa Kitanzania wanaweza kuchangamkia ikiwemo za uhudumu, wapishi wa melini, na nafasi za mabaharia wote katika kada za uongozaji meli na mitambo.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa Kampuni yake inataka Watanzania wazalendo, wenye nidhamu, maadili, wachapakazi, wenye weledi na wanaofanya kazi kwa bidii na ushirikiano.
Aidha, Bi. Mutaki, amewashukuru kwa ujio wao, na kuwaahidi kuwa TASAC ipo tayari kutoa ushirikiano katika kila hatua ili kuhakikisha mabaharia wa Kitanzania wanafaidika na fursa hizo za ajira.
Mkurugenzi Mutaki ametoa wito kwa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na vyuo vinavyotoa mafunzo kwa mabaharia husan Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ili kuhakikisha wanaendelea kutoa wahitimu wenye viwango vya kimataifa ili waweze kunufaika na fursa hizo.