TASAC yaipongeza TPA Nyamisati
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Nah. Mussa Mandia imeipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kutekeleza vema maelekezo ya kudhibiti usalama wa abiria na mizigo katika bandari ya Nyamisati.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Nah. Mussa Mandia leo tarehe 23 Julai, 2024, wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye ziara ya ukaguzi bandari ya Nyamisati, wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.
"TPA hongera sana kwa kutekeleza maelekezo yetu ya Mwaka 2022 tulipofanya ziara hapa na kuelekeza TPA kuweka utaratibu mzuri wa abiria kuingia kwenye meli, kujenga jengo la kutunzia mizigo na kutenganisha mizigo ya vyakula na mizigo mengine. Yote yametekelezwa na mengine yanaendea kutekelezwa. Hakika tumefurahi kuona maboresho hayo", amesema Nah.Mandia.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema bandari hii ni moja ya bandari ndogo zinazofanya vizuri katika kutoa huduma ya usafiri.
"Kwa ujumla maelekezo ya bodi yametekelezwa na imetuelekeza tuendelee kusimamia uboreshaji wa eneo la bandari lenye udongo linalolika kwa maji kwa kuwekwa tabaka gumu ili maji yasiendelee kuondoa udongo. Nasisi tutalisimamia hilo."
Bandari ya Nyamisati inatoa huduma kwa zaidi ya visiwa 16 kwa kupeleka mizigo ya vyakula, mavazi,vifaa vya ujenzi na mengineyo.
Naye Meneja wa bandari Nyamisati, Bw. Issa Unemba amesema kuwa bandari hii ni ya kimkakati katika kuhudumia visiwa vya bahari Hindi. Hivyo wamefanya maboresho mengi bandari hapo na wataendelea kuboresha zaidi kwa kuwa vifaa vya kupakia na kupakua mizigo.
"Kama mnavyoona mabadiliko mengi yamefanyika. Bandari yetu imejidhatiti katika kuwahudumia wananchi. Maelekezo ya bodi tumeyatekeleza na tunashukuru sana na tunafarijika kwa ujio wenu tena", amesema Meneja wa Bandari Nyamisati, Bw..Issa Unemba.
Bandari hii inahudumia meli tatu, na vyombo vidogo vya usafiri majini.Kwa mwaka inasafirisha abiria zaidi 4000 na mizigo zaidi ya tani 200 kwa mwezi.
Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC imeendelea na ratiba ya ziara yake katika mkoa wa Pwani .