TASAC yailekeza TPA kufuata sheria na kanuni za Usalama wa Usafiri Majini
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ikiongozwa na Nah. Mussa Mandia leo tarehe 22 Julai, 2024 imefanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za udhibiti wa usafiri majini katika wilaya ya Mafia Mkoani Pwani na kuitaka Mamlaka ya Bandari (TPA) kufuata sheria na kanuni za Usafiri Majini.
Akizungumza katika ziara hiyo Nah. Mandia ameilekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufuata Sheria na Kanuni za usalama wa usafiri majini katika kutoa huduma ya usafiri katika bandari ya kilindoni kisiwani Mafia.
“TASAC ni mdhibiti na kuna sheria na kanuni tunazisimamia, wenzetu TPA ni watekelezaji, inatubidi tuwakague mara kwa mara na kuwaelekeza wapi pa kurekebisha ili kuondoa kasoro hizi ndogo na hatarishi. Fikirieni kuwa na maboya ambayo ikitokea dharula mtu kutumbukia anarushiwa boya” amesema Nah.Mussa.
Aidha, amehimiza ushirikiano baina ya taasisi nyingine hususan inapotokea dharula kwani suala la usalama ni jukumu la vyombo vyote vya serikali, wavuvi na wananchi.
Akikagua ghati ya kuhudumia Meli za abiria na mizigo Nah. Mussa amesema ghati hilo linahitaji ukarabati mkubwa kwani mbao zake zimelegea, nyavu za uzio wa pembeni mwa ghati zimechanika na hakuna vifaa vya kujiokolea.
"Ghati hili linahitaji ukarabati mkubwa kwani mbao zake zimelegea, nyavu za uzio wa pembeni mwa ghati zimechanika na hakuna vifaa vya kujiokolea. Hivyo, wazamiaji mara inapotokea dharula inaweza sababisha mtu au mizigo kutumbukia kwenye maji maana kuna wakati hali ya bahari inakuwa sio shwari." Amesema Nah. Mandia.
Ziara hii ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC imeanza leo tarehe 22 Julai, 2024 katika Wilaya ya Mafia, itafutia Nyamisati, Bagamoyo na kuishia tarehe 27 Julai, 2024 katika mwalo wa mkwaja mkoani Tanga.