TASAC YAIBUKA MIONGONI MWA WASHINDI WA TUZO YA MAZINGIRA CHALLENGE 2026
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeibuka mshindi wa nne wa Tuzo ya Mazingira Challenge 2026 iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ikiwa ni kutambua mchango wake katika kulinda mazingira ya usafiri majini na kuendeleza uchumi wa buluu.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba). Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Stanslaus Muyungi, alimkabidhi tuzo hiyo ilipokelewa na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TASAC, Bi. Amina Miruko, kwa niaba ya Shirika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Muyungi amesema Serikali imendelea kuweka kipaumbele katika utunzaji na uhifadhi mazingira kupitia uwekezaji wa kijani, biashara endelevu na usimamizi bora wa rasilimali za asili. Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika uhifadhi wa misitu, ambayo sasa inakadiriwa kufunika takribani hekta milioni 48.1, sawa na asilimia 38 ya eneo la nchi.
Ushindi huo unaakisi jitihada za TASAC katika kusimamia usalama, ulinzi na uhifadhi wa mazingira ya usafiri majini kupitia utekelezaji wa sheria, kanuni na mikataba ya kimataifa ya mazingira ya baharini. Aidha, Shirika linaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na maziwa kwa lengo la kuimarisha uchumi wa buluu na kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika sambamba na kumbukumbu ya miaka 40 ya NEMC tangu kuanzishwa kwake, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, "Tunza Mazingira, Linda Taifa."