Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MHE. JAFO AIPONGEZA TASAC KWA KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI

Imewekwa: 13 July, 2026
MHE. JAFO AIPONGEZA TASAC KWA KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI

Jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuendelea kuimarisha sekta ya usafiri na uchukuzi kupitia uwekezaji katika miundombinu, kuimarisha taasisi za umma na kuweka mazingira wezeshi ya utoaji huduma, zimeendelea kuleta matokeo chanya yanayoonekana katika maendeleo ya sekta mbalimbali, ikiwemo usafiri wa majini.

 

Katika kuunga mkono juhudi hizo za Serikali ya Awamu ya Sita, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Mhe. Suleiman Jafo, ameipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kazi kubwa na yenye mafanikio inayofanya katika kusimamia, kudhibiti na kuendeleza sekta ya usafiri wa majini nchini.

 

Mhe. Jafo ametoa pongezi hizo leo, Julai 12, 2026, alipotembelea banda la TASAC katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo pamoja na elimu inayowafikia wananchi kuhusu sekta ya usafiri wa majini.

 

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Jafo amesema TASAC imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi katika kusimamia usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira katika sekta ya usafiri wa majini pamoja na  kusimamia biashara za meli na kuhakikisha sheria na kanuni za sekta hiyo zinazingatiwa.

 

Aidha, Mhe. Jafo amesema TASAC ina nafasi muhimu katika kuimarisha uchumi wa buluu kupitia usimamizi madhubuti wa sekta ya usafiri wa majini, na kuwataka watumishi wa shirika hilo kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma ili kuongeza ufanisi wa huduma, kuimarisha usalama na ulinzi wa usafiri wa majini, pamoja na kuendelea kutoa mchango katika kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania.

 

TASAC inashiriki Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi kuhusu majukumu yake na mchango wake katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na usafiri majini ulio salama na endelevu.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo