MWENYEKITI WA MACHIFU TANZANIA AJIONEA HUDUMA ZA TASAC SABASABA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea kupokea viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA). Miongoni mwa viongozi hao ni Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Bi. Antonia Sangalali, ambaye amejionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika katika kuimarisha usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira katika sekta ya usafiri wa majini.
Akiwa katika banda hilo, Bi. Sangalali ameelezwa majukumu ya TASAC yakiwemo kusimamia usalama wa usafiri wa majini, kusajili na kutoa vyeti kwa mabaharia, kusimamia biashara za meli, pamoja na maboresho yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha huduma za utafutaji na uokoaji (SAR).
Bi. Sangalali ameeleza kufurahishwa na kazi inayofanywa na TASAC katika kusimamia sekta ya usafiri wa majini na kutoa elimu kwa wananchi amesema huduma hizo zina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu usalama wa usafiri wa majini, kulinda mazingira ya bahari, maziwa na mito, pamoja na kuhimiza uzingatiaji wa sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo.
Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayarajiwa kufungwa rasmi tarehe 13 Julai, 2026 na kukamilika Tarehe 14 Julai 2026, ambapo TASAC inaendelea kushiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo.