TASAC YAFANYA UKAGUZI CHUO KIPYA CHA MAFUNZO YA UBAHARIA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kupitia Mkurugenzi Mkuu ambae pia ni Msajili wa Mabaharia Bw. Mohamed Salum amefanya ukaguzi wa miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Mafunzo ya Awali ya Ubaharia Cha Dar es Salaam - Dar es Salaam Maritime Training Academy (DMTA) kilichopo mtaa wa Nkurumah jijini Dar Es salaam.
Aidha, chuo hicho kimeomba kupewa ithibati ya kufundisha kozi za awali za ubaharia (Basic Safety Training).
Tasnia ya ubaharia nchini imepata msukumo mpya kwa sekta binafsi kuanzisha vyuo kwa ajili ya kuongeza ujuzi wa awali katika masuala ya usafiri majini.
Bw. Salum amesema kuwa, Tanzania kuna kundi kubwa la vijana ambao wakitumia fursa ya kujiunga na DMTA itasaidia kujenga safari mpya ya maisha yao.
“Tanzania tuna bahari na maziwa ambayo tukiyatumia vema yatachangia kuongeza ajira kwa vijana na kupunguza ukosefu wa ajira. Hongereni sana uongozi wa DMTA kwa kuanzisha chuo hiki, aidha, natoa wito kwa watanzania wenye uwezo wa kuanzisha vyuo kama hivi wajitokeze na kuanzisha vyuo hivyo katika maeneo ya ziwa Victoria, Tanganyika na mengineyo”, amesema Bw. Salum.
Chuo hicho kitakuwa na kozi fupi na kitaendeshwa kwa mitaala inayokidhi miongozo ya Shirika la Bahari Duniani (IMO) pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Viwango vya Mafunzo, Utoaji wa Vyeti na Ulinzi wa Mabaharia “International Convention on Standards of Training, Certification and Watchkeeping for Seafarers (STCW)1978 as amended”
TASAC imeridhishwa kwa hatua hizo za awali na sasa mchakato wa mwisho unaendelea ili kipewe ithibati ya kuanza rasmi mafunzo hayo