Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAFANYA MAJADILIANO NA KMA KUHUSU KUFANYA MAZOEZI YA UTAYARI

Imewekwa: 10 March, 2025
TASAC YAFANYA MAJADILIANO NA KMA KUHUSU KUFANYA MAZOEZI YA UTAYARI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekutana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Majini ya Kenya (KMA) na kufanya majadiliano namna  ya kushirikiana kufanya zoezi la utayari wa kupambana na umwagikaji wa mafuta baharini litakalofanyika Mombasa nchini Kenya mwezi Julai, 2025.

Wakiwa katika ziara yao nchini Tanzania, ugeni kutoka KMA uliambatana Mjumbe kutoka Tume ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Commission-(IOC) ulitembelea ofisi zs TASAC, tarehe 5 Machi, 2025 na kupokelewa na Naho. Alex Katama, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC.

Akizungumza na wageni hao Nahodha Katama amesema ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ni muhimu katika sekta ya uchukuzi majini ili kuendelea kutumia vyema fursa  za uchumi wa bluu. Aliongeza kuwa ili kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika sekta hii, inabidi kujenga uwezo wa utayari wa kupambana na umwagikaji wa mafuta kwenye bahari.

"Tumekutana pamoja kuona uwezekano wa kutumia wataalam  na vifaa tulivyo navyo, kusafishia mafuta endapo yatamwagika (Oil spill)  kama sehemu ya maandalizi ya kufanya zoezi la kikanda la  kupambana na umwagikaji wa mafuta baharini  litakalofanyika Julai, 2025 katika Kaunti ya Mombasa nchinIi Kenya," amesema Naho. Katama.

Ugeni huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Usalama wa Usafiri Majini KMA, Mha. Julius Koech akiwa ameambatana na Mtaalam kutoka IOC, Bw. Roman Chancerel.

Ugeni huo uliishukuru TASAC kwa kuridhia kuendesha zoezi la utayari la kupambana na umwagikaji wa mafuta baharini ambapo wamekubaliana kufanya vikao vya pamoja ili kuweka nguvu katika kuhakikisha bahari inakua salama wakati wote.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo