Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAFANYA KAGUZI KWENYE MELI ZA KIGENI

Imewekwa: 09 January, 2025
TASAC YAFANYA KAGUZI KWENYE MELI ZA KIGENI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limefanya kaguzi kwenye meli mbalimbali ikiwemo meli ya Haima Panama na kujiridhisha iwapo inafanya kazi kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, tarehe 07 Januari, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkaguzi wa TASAC, Mhandisi Samwel Chubwa, amesema kuwa TASAC  inafanya kaguzi hizo ili kujiridhisha iwapo uendeshaji wa meli zote zinazoingia nchini zinakidhidhi viwango vya vya kimataifa.

"Zoezi hili la ukaguzi ni endelevu na tunao wajibu wa kisheria kukagua meli  zinazokuja katika bandari zetu ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya kimataifa. Baada ya kuikagua meli hii ya Haima Panama tumejiridhisha kuwa imekidhi viwango vinavyotakiwa na tumeipatia cheti safi," amesema Mha. Chubwa.
Aidha, Mha. Chubwa amesema kuwa TASAC imeongeza nguvu za kufanya kaguzi kwenye meli meli zote zinazoingia nchini kutokana na kuwa na boti ya doria inayorahisisha utendaji wa kazi katika Bahari ya Hindi.

Boti hiyo ya Doria  ambayo ilikabidhiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21 April, 2024 kupitia kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania chini ya Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu nchini, inaendelea kutekeleza majukumu yake katika ukanda wa pwani ya Tanzania. 

Boti hiyo ambayo ni ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kufanya doria kwa muda mrefu, imeongeza ufanisi katika suala la Ulinzi katika maji ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Kuimarika kwa Usalama wa “Single Point Mooring (SPM) na Visiwa vidogo vinavopatikana nje kidogo ya mlango wa kuingilia katika Bandari ya Dar es Salaam.

TASAC inaendelea na ukaguzi, zoezi hili ni endelevu na hufanywa kwa nchi nzima ili kuhakikisha wamiliki na waendesha vyombo vya usafiri majini wanazingatia sheria na kanuni zilizowekwa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo