TASAC YAENDELEA NA KAGUZI ZAKUSHITUKIZA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 18 Agosti, 2025 limeendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye vyombo vya usafiri majini (boti) zinazofanya safari kati ya Dar es Salaam na Zanzibar katika bandari ya abiria iliyopo jijini Dar es Salaam.
Zoezi hili limevihusisha vyombo vya Zanzibar Fast Ferries na Azam Marine likiwa na lengo la kuhakikisha usafiri majini unakuwa salama na kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa kwa usalama wa abiria na mali zao.
Ukaguzi huo umehusisha ukaguzi wa nyaraka mbalimbali za boti, mabaharia, idadi ya abiria wanaopanda, vifaa vya usalama na taratibu nyingine za usafirishaji na ulinzi.
Zoezi hilo liliongozwa na Mha. Lameck Sondo Kaimu Meneja wa Huduma za Mafunzo ya Ubaharia na Utoaji Vyeti kwa Mabaharia, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri Majini na Utunzaji wa Mazingira.
Katika ziara hiyo, timu ya ukaguzi ilibaini kuwa Zan Ferries na Azam Marine zimeendelea kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni zote za usalama na usafirishaji majini.
"Tumeridhishwa na matokeo ya ukaguzi huu na nasisitiza kuwa TASAC tutaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini," amesema Mha.Sondo.
Mha. Sondo amewataka wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri majini kuendelea kutii sheria bila kusubiri kaguzi za kushtukiza, kwa kuwa usalama wa abiria ni kipaumbele cha kwanza cha Serikali.