Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC yaelezea mafanikio yake Miaka Miwili ya Mh. Dkt. Samia Madarakani

Imewekwa: 22 March, 2023
TASAC yaelezea mafanikio yake Miaka Miwili ya Mh. Dkt. Samia Madarakani

Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania  (TASAC) inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria ili kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri majini na uvuvi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge leo Jijini Dodoma wakati akieleza mafanikio ya miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita na tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka  2018 ikiwa na lengo la kuboresha sekta ya usafiri majini.

“Lengo la mradi huu pamoja na mambo mengine ni kujenga vituo vinne  vya uokozi ambapo vitakuwa katika maeneo ya Kanyala – Sengerema, Musoma - Mara, Nansio - Ukerewe na Ilemela – Mwanza  ambavyo vitasaidia katika kushughulikia changamoto za usafiri kwa njia  maji na katika uokozi majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri kwa njia maji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria”, amefafanua Bw. Mkeyenge. 

Aidha, amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda na umepangwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za mradi ni shilingi bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda. 

Akizungumza kuhusu mafanikio ya Taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkuu huyo amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewezesha kuongezeka kwa mchango  katika Mfuko Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka kutoka shilingi bilioni 9.1 mwaka wa fedha 2018/19 hadi kufikia shilingi bilioni 43.5 mwaka wa fedha 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 21 na hivyo kufanya jumla ya mchango wa TASAC katika mfuko mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka minne kuwa shilingi bilioni 104.5.

Vilevile, TASAC imewezesha kuongezeka kwa idadi ya watoa huduma wanaodhibitiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 idadi ya leseni na vyeti vya usajili imefikia 1,195 ikilinganishwa na leseni na vyeti vya usajili 941 katika mwaka wa fedha 2018/19 sawa na ongezeko la asilimia 79.

 “ Pia TASAC imewezesha ongezeko la idadi ya vyeti vya mabaharia waliokidhi masharti kutoka 6,068 katika mwaka 2018/19 hadi kufikia 19,575 katika mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 31 ”, ameongeza Bw. Mkeyenge.

Mbali na hayo TASAC inajivunia kuimarisha usimamizi wa usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira dhidi ya shughuli za meli kwa lengo la kupunguza matukio ya ajali za vyombo vya majini ambapo kaguzi 6,208 za vyombo vya usafiri majini zilifanyika katika mwaka wa fedha 2021/22 na kaguzi 4,490 katika kipindi cha Julai 2022 hadi ifikapo mwezi Juni 2023 matarajio ni  kufikia vyombo takriban 8,000.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo