TASAC NA ZMA ZATOA MAFUNZO KWA WAKAGUZI WA MELI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikia na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) wameratibu mafunzo ya Tathmini ya Hali ya hewa kwa wakaguzi wa Meli ili kuwajengea uwezo pindi wanapofanya kaguzi katika meli za kimataifa na za kitaifa.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar Bw. Yasin Thabit ambae ni Mkurugenzi wa Idara ya Usajili wa Meli na Mabaharia leo tarehe 13 Januari 2026 katika Hoteli ya Golden Tulip - Zanzibar amesema kuwa, mafunzo hayo yana lengo la kujifunza kutoka kwa wenzetu na kuona ni nini ambacho tunakikosa kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani.
“Lengo la TASAC na ZMA ni kuwawezesha wakaguzi wetu wa meli kujifunza kuhushu mbinu mpya za ukaguzi wa meli kwani teknolojia ya leo si kama ilivyokuwa miaka 20 iliyopita na miongozo ya kimataifa kutoka Shirika la Bahari Duniani (IMO), hivyo tunaka twende kwa namna ambavyo dunia inakwenda katika masuala mazima ya ukaguzi wa meli. Amesema Bw. Yasin.
Pia ameongeza kuwa kutokujifunza kutoka kwa wenzetu kutatengeneza utofauti wa kitaalamu kwetu na wenzetu ambao wameendelea zaidi katika masuala haya ya ukaguzi kwa kuwa kaguzi hizi zinafanyika kwa utaratibu na miongozi kutoka Shirika la Bahari Duniani kwa nchi zote.
Kwa Upande wake Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti vya Mabaharia (TASAC) Mha. Lameck Sondo amewashukuru wawezeshaji kutoka Chuo cha Kimataifa cha Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira cha Italia (IMSSEA) kwa kukubali kuja kutoa mafunzo hayo nchini Tanzania kwa wakaguzi wa meli na kuwaasa washiriki kushiriki kikamilifu ili kuleta tija kwa nchi.
Jumla ya wakaguzi wa meli 25 kutoka TASAC na ZMA wanashiriki mafunzo hayo ya siku 4 kuanzia tarehe 13 hadi 16 Januari 2026 kutoka kwa wawezeshaji wabobezi wa kimataifa katika masuala ya usafiri kwa njia ya maji kutoka IMSSEA