TASAC NA NBS WAANZA MAANDALIZI YA SENSA YA VYOMBO VYA USAFIRI MAJINI NA WAJENZI WA MELI 2026/27
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania leo, tarehe 13 Februari 2026, limekutana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuanza maandalizi ya Sensa ya Vyombo vya Usafiri Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara, itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27.
Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za TASAC, Jengo la Golden Jubilee, jijini Dar es Salaam, ambapo pande zote mbili zimejadili mikakati ya kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi, weledi na kuleta matokeo chanya kwa sekta ya usafiri wa majini nchini.
Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, amesema sensa hiyo inalenga kutambua na kuorodhesha vyombo vyote vya usafiri majini pamoja na wajenzi wa meli ili kupata takwimu sahihi, za kuaminika na zenye kukidhi mahitaji ya kitaifa.
Ameeleza kuwa takwimu hizo zitawezesha Serikali kusimamia kwa ufanisi sekta ya usafiri wa majini, kubainisha mchango wake katika ukuaji wa uchumi, pamoja na kutambua fursa na changamoto zilizopo kwa ajili ya kupanga mikakati madhubuti ya maendeleo ya taifa.
“Lengo la sensa hii ni kuwa na takwimu sahihi zitakazosaidia kuboresha usimamizi wa sekta na kuwezesha upangaji wa mipango thabiti ya maendeleo,” amesema Bw. Salum.
Aidha, ameongeza kuwa sensa hiyo itasaidia kuhuisha na kuimarisha kanzidata ya vyombo vidogo vya usafiri majini na wajenzi wa meli, hatua itakayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa matumizi mbalimbali ya kiutawala, kiuchumi na kiusalama.
Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa NBS, Dkt. Amina Msengwa, amesisitiza umuhimu wa kupanua wigo wa sensa hiyo ili kujumuisha taarifa za kina zitakazochochea upangaji bora wa sera na mipango ya maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini na taifa kwa ujumla.
Ameipongeza TASAC kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha takwimu za sekta hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili utaongeza ubora, uhalali na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi sahihi kwa maendeleo endelevu ya nchi.