Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC NA IMO ZAWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 19 August, 2025
TASAC NA IMO ZAWAJENGEA UWEZO WATAALAM WA USAFIRI MAJINI

Shirika la Uwakala Wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Shirika la Bahari Duniani (IMO), leo tarehe 18 Agosti, 2025 wameanza mafunzo ya siku tano ya kuangalia tathmini ya usalama wa miundombinu ya usafiri majini. 

Akiongea katika ufunguzi wa warsha hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Bi Stella Katondo amesema sekta ya usafiri wa majini ni muhimu katika kujenga uchumi wa nchi, hivyo, ni muhimu kuwa na wataalam wabobezi wa kufanya tathmini za usalama katika bandari nchini.

Ameongeza kuwa warsha hiyo inatia ujuzi wa kiufundi na wa kiutendaji pamoja na nyenzo za kutambua, kushughulikia na kupunguza mianya ya kihalifu iwe katika mifumo ya kiutendaji au maeneo mengine muhimu kwa uendeshaji bandari zetu.

Naye Mkurugenzi wa Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira TASAC Wakili Leticia Mutaki kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu amesema  kuwa TASAC inaishukuru IMO kwa kuendelea kutoa mafunzo yanayosaidia kuimarisha usalama wa bandari kwa lengo la kuboresha na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafiri majini pamoja na kujengea watumishi uwezo wa kufanya tathmini ya usalama wa bandari kwa weledi zaidi. 

Kwa upande wake Mwakilishi wa IMO, Bi. Ivy Kamande amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuibua  mbinu mpya na vifaa vya kutendea kazi katika kufanya tathmini ya usalama wa miundombinu ya bandari  kuanzia kutambua hatari za kimwili na kimuundo, pamoja na tathmini ya mifumo ya usalama wa wafanyakazi, mawasiliano ya simu, na sera za kiutendaji, kupitia  mazoezi, na majadiliano ya moja kwa moja katika warsha hii. 

"Mafunzo haya yanalenga kuimarisha utayari wa kitaasisi na kuunga mkono juhudi za Tanzania za kulinda milango yake ya bahari," amesema.

Mafunzo hayo yanafanyika katika Hoteli ya Four Point ya Jijini Dar es Salaam yanawashirikisha wadau kutoka Wizara ya Uchukuzi, TASAC, Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya usafiri majini. 

Mafunzo hayo yaliyoanza leo tarehe 18 Agosti, 2025 yatahitimishwa tarehe 22 Agosti, 2025.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo