TASAC, MSALABA MWEKUNDU WATOA ELIMU YA UOKOAJI KIGOMA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania, limetoa elimu ya uokoaji na usalama majini kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendelea kupunguza ajali zinazotokea katika maeneo ya maji nchini.
Elimu hiyo imetolewa kupitia mafunzo kwa vitendo na nadharia yaliyowahusisha wavuvi, waendesha vyombo vya majini, wanafunzi pamoja na wananchi wanaotumia usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kigoma, Nahodha Adam Mamilo, amesema TASAC inaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya usalama majini kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa kabla na wakati wa safari za majini.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi uwezo wa kutoa msaada wa haraka pale ajali zinapotokea, ikiwemo namna ya kufanya uokoaji wa awali, matumizi sahihi ya vifaa vya kujiokoa pamoja na hatua za kuzingatia ili kuzuia madhara makubwa.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Msalaba Mwekundu Tanzania, Bw. Exavery Eustarch amesema mafunzo hayo yamejikita pia katika huduma ya kwanza kwa waathirika wa ajali za majini na namna ya kushughulikia dharura kabla ya wahusika kufikishwa katika vituo vya afya.
Wananchi walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru TASAC na Msalaba Mwekundu kwa kuwapatia elimu muhimu inayosaidia kuokoa maisha na kuongeza usalama katika shughuli zao za kila siku zinazotegemea usafiri majini.
Nahodha Mamilo amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za usalama majini, ikiwemo matumizi ya vifaa vya kuokoa maisha, ili kuhakikisha safari za majini zinafanyika kwa usalama wakati wote.