TASAC KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAWAKALA WA MELI ZA MWAMBAO WA BAHARI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 16 Oktoba, 2025 limefanya kikao na Mawakala wa Meli za Mwambao wa Bahari ziendazo Zanzibar na Visiwa vya Comoro (Coastal Vessel Agents) katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Jengo la SUMATRA jijini Dar es Salaam, ili kujadili changamoto zinazohusiana na masuala ya usafiri majini.
Akizungumza kwenye kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Sylvester Kanyika, Afisa Mkuu wa Udhibiti na Usafirishaji Majini kutoka TASAC ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho amewataka wadau kushirikiana na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ili kuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Bw. Kanyika amesema kuwa kupitia kikao hicho kuna changamoto zimetatuliwa na kuongeza kuwa kwa changamoto zilizokosa ufumbuzi zitafanyiwa kazi ipasavyo.
“Niwaombe wadau kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake ili kuweza kufanikisha kazi, lakini pia kupunguza changamoto zinazoweza kutatulika kwa kutekeleza wajibu," amesema Bw. Kanyika.
Aidha, Bw. Kanyika amewashukuru wadau kwa kujitokeza kushiriki kikao hicho na kuwaomba kuwa na ushirikiano mzuri katika kazi ili kutekeleza majukumu kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
"Nipende kutoa shukrani zangu kwa muitikio wenu, hii inaonesha tunakwenda pamoja, naomba mwitikio wa mahudhurio haya uendelee katika vikao vijavyo," amesema Bw. Kanyika
Kwa upande wao wadau wa usafiri majini wameshukuru kwa kufikia muafaka wa changamoto zilizokuwepo, na kuwaomba kutochukua muda mrefu kutatuliwa kwa changamoto zilizokosa ufumbuzi.
Baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho ni Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), DP World, Tanzania East Africa Gateway Terminal (TEAGL) na Mawakala wa Meli za Mwambao wa Bahari (Coastal Shipping Agents)