TASAC KUSHIRIKIANA NA PMAESA KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI MAJINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 12 Agosti, 2025 limekutana na Chama cha Usimamizi wa Bandari Mashariki na Kusini mwa Afrika (PMAESA) kwa lengo la kujadili ushirikiano katika masuala yanayohusu ushirikiano wa kikanda katika usimamizi wa bandari, usalama na utunzaji wa mazingira ya bahari.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa TASAC uliopo Golden Jubilee, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum aliwashukuru PMAESA kwa kutembelea Tanzania pamoja na kuonesha dhamira ya taasisi hiyo kushirikiana kwa karibu na TASAC.
“Tunashukuru sana kwa kutembelea na tumeona dhamira yenu ya kushughulikia changamoto za sekta ya usafiri majini ikiwemo msongamano katika bandari, gharama za usafirishaji, kanuni za usalama pamoja na utunzaji wa mazingira,” alisema Bw. Salum.
Alieleza baadhi ya jitihada za hivi karibuni za TASAC katika kuboresha miundombinu ya bandari ni pamoja na urahisishaji wa taratibu za kushughulikia mizigo, ambazo zinaweza kuwa mfano bora kwa bandari nyingine za ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Naye Katibu Mkuu wa PMAESA, Kanali André Didace Ciseau aliipongeza TASAC kwa uongozi na maono yake katika sekta ya baharini na kubainisha kuwa ushirikiano kati ya nchi wanachama ni muhimu katika kuunda sekta ya usafirishaji yenye ushindani na endelevu katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Kanali Ciseau alisisitiza nafasi ya PMAESA katika kuwezesha kubadilishana uzoefu, kuratibu sera, na kuendesha programu za kujenga uwezo ambazo zitawanufaisha washiriki wote wa bandari na mashirika ya usafirishaji yaliyo katika mtandao wake.
Mkutano huo ulimalizika kwa maazimio ya pamoja yaliyobainisha maeneo ya ushirikiano, yakiwemo mabadiliko ya kidijitali katika uendeshaji wa bandari, ulinzi na utunzaji wa mazingira, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi. Pia, TASAC na PMAESA ziliahidi kuendeleza vikao vya mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo na kubadilishana mbinu bora za kiutendaji.