Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA 8 WA AAMA NCHINI LIBERIA

Imewekwa: 01 October, 2025
TANZANIA YASHIRIKI MKUTANO WA 8 WA AAMA NCHINI LIBERIA

Tanzania imeungana na viongozi wa usafiri wa majini barani Afrika pamoja na wadau wa Kimataifa katika Mkutano wa 8 wa Chama cha Mamlaka za Usimamizi wa Masuala ya Baharini Afrika (AAMA), unaofanyika kuanzia tarehe 30 Septemba hadi 3 Oktoba 2025 katika Jengo la EJS Ministerial Complex, Mjini Monrovia.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Mhe. Samuel  Stevquoah, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Liberia, kwa niaba ya Rais Joseph Nyuma Boakai. Katika hotuba yake, Mhe. Stevquoah alisisitiza umuhimu wa kaulimbiu ya mwaka huu: “Kulinda Bahari Yetu, Kukuza Utengaji wa Kaboni Katika Usafirishaji Majini, kuchunguza Uwezo wa Uchumi wa Buluu Afrika.” Alieleza dhamira ya pamoja ya Afrika katika kuhakikisha usafiri endelevu wa majini na kufungua fursa za uchumi wa buluu.

Mkutano huo umewakutanisha mawaziri, wasimamizi wa sekta ya bahari, mashirika ya kikanda, na wataalam wa kimataifa kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu  masuala ya usimamizi wa  bahari, usalama na ulinzi wa mazingira ya baharini, na kuendeleza maslahi ya Afrika katika usafiri wa majini kimataifa.

Ajenda kuu za mkutano huo ni juu ya mafanikio ya Mkutano wa 7 wa AAMA uliofanyika nchini Tanzania. Majadiliano yaliyojumuisha:
Ufadhili wa uchumi wa buluu endelevu Afrika,
Usafiri wa majini na urahisishaji wa biashara,
Utawala bora, Uimarishaji uwezo wa Usalama na Ulinzi wa mazingira, Usafirishaji wa kijani kwa usawa na utofauti katika sekta ya bahari.

Aidha, mkutano huo unajadili usalama wa vivuko ndani ya  bara la Afrika, ukihimiza mamlaka za baharini kuzingatia mwongozo wa Shirika la Bahari Duniani (IMO) kuhusu kanuni na miongozo ya usalama kwa vivuko vya ndani.

 Lengo ni kuboresha usalama wa abiria, kuoanisha mifumo ya kisheria, na kupunguza hatari katika uendeshaji wa vivuko barani kote.

Tanzania inawakilishwa na ujumbe unaoongozwa na Wakili Leticia Mutaki kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), akihudhuria kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC. Taasisi nyingine zinazoshiriki ni pamoja na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Mamlaka ya Bahari Zanzibar (ZMA), wakionesha mshikamano katika elimu, udhibiti na uundaji sera za baharini.

Akizungumza katika mkutano huo, Wakili Mutaki alisisitiza kuwa Tanzania imejikita katika ushirikiano wa kikanda katika kushughulikia changamoto  uzalishaji hewa ya kaboni, usalama na ukuaji wa uchumi wa buluu. Alieleza kuwa mikakati ya Tanzania ni kupanua miundombinu ya bandari kuifanya nchi kuwa na nafasi ya kipekee katika kukuza ukuaji wa uchumi bluu barani Afrika na kulinda mazingira ya kijani

Kupitia ushiriki wake, Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake katika kuunda sera za usafiri majini barani Afrika, huku ikionesha uongozi katika biashara endelevu, ubunifu na ushirikiano wa kikanda kupitia bahari.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo