TANZANIA NA KENYA ZASAINI MAKUBALIANO MUHIMU KUIMARISHA SEKTA YA USAFIRI MAJINI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imesaini Hati za Makubaliano kuhusu Kutambuliana Vyeti vya Ubaharia na Usimamizi wa Sekta ya Usafiri kwa njia ya Maji na Serikali ya Jamhuri ya Kenya kupitia Mamlaka ya Usafiri Baharini Kenya (KMA).
Hafla hiyo imefanyika leo tarehe 4 Mei, 2026 katika Ikulu ya Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Dkt. William Samoei Ruto.
Makubaliano haya yanatarajiwa kuongeza fursa za ajira kwa mabaharia wa Tanzania na Kenya, pamoja na kukuza ushindani na uhamaji wa wataalamu katika sekta ya usafirishaji majini, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya miundombinu ya bandari, usalama wa usafiri majini, ulinzi wa mazingira ya bahari, na kubadilishana uzoefu na teknolojia kati ya nchi hizo mbili.
Kupitia makubaliano haya, Tanzania na Kenya zinatarajia kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri majini, kurahisisha biashara ya kikanda, na kuchochea ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha usimamizi madhubuti wa sekta ya usafiri majini, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.