Tanzania lango la Uchumi wa nchi 7
Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB) , Waziri wa Uchukuzi amesema serikali inajenga na kuboresha miundo mbinu ya uchukuzi na kufanya mabadiliko ya kimkakati katika Sekta ya Uchukuzi ili kuifungua nchi na Mataifa mengine.
Hayo yamesemwa na Mhe. Prof. Mbarawa leo tarehe 14 Agosti, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana jijini Dar es salaam wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Uchukuzi na lojistiki wa Afrika Mashariki wenye kauli mbiu "Tasnia ya ugavi na lojistiki Afrika Mashariki".
"Serikali inapowekeza katika kupanua na kujenga bandari, reli, bandari za maziwa na kuboresha sera na sheria inaongeza fursa kwa wananchi wake, sekta binafsi nashauri mjiunge pamoja ili muwekeze zaidi katika kuvuna fursa hizi." Amesema Mhe. Prof. Mbarawa
Lengo la Mkutano huo ni kubadishana uzoefu, utaalam na kujenga ushirikiano wa pamoja katika Sekta ya Uchukuzi na lojistiki, lakini pia kubadilishana uzoefu, kushirikiana kwa wataalam wa lojistiki, kuwa na majadiliano ya wakati ujao na kuwezesha mazingira ya watunga Sera na Sheria kupata taarifa ya kuboresha Sera na kufanya maamuzi ya kuwa na uchukuzi endelevu.
Aidha, Mkutano huo unajumuisha nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya, Tanzania na nchi za Afrika ya kati.
Mkutano huo ambao Tanzania ndio nchi mwenyeji ulianza kufanyika mwaka 2017 hapa nchini na hufanyika kila mwaka kwa nchi wanachama.