Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Baraza la Usafirishaji Tanzania (TSC) pamoja na ISCOS limefanya Mkutano wa kuelimisha wasafirishaji wa Shehena Njombe.

Imewekwa: 28 April, 2023
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Baraza la Usafirishaji Tanzania (TSC) pamoja na ISCOS limefanya Mkutano wa kuelimisha wasafirishaji wa Shehena Njombe.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Baraza la Usafirishaji Tanzania (TSC) pamoja na ISCOS limefanya Mkutano wa kuelimisha wasafirishaji wa Shehena (Shippers) tarehe 17 Aprili, 2023 Mkoani Njombe.

Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Kisa Kasongwa amesema Uchumi wa Mkoa wa Njombe umekuwa ukikuwa kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi hususani katika sekta ya kilimo.

Aidha, Mhe. Kasongwa ameongeza kuwa licha ya mafanikio makubwa ya Mkoa huo, uchumi wa Mkoa na nchi kwa ujumla hauwezi kukua bila ya kuwa na ufanisi katika shughuli za usafiri majini kwa kusafirisha bidhaa nje ya nchi kwa njia ya bandari itapelekea nchi kupata fedha za kigeni sanjari na kuongeza pato la Taifa.

"Tumeshuhudia maboresho ya bandari zetu nchini zinazopelekea kuimarika kwa huduma za usafirishaji majini na kukuza uchumi wa Mkoa wa Njombe na nchi kwa ujumla." Alisema Mhe. Kasongwa.

Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania Bw. Deogratious Mukasa amesema Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano inayofanyika katika maeneo ya kimkakati kwa kutoa fursa kwa TASAC na wadau kujadili changamoto na kuja na suluhisho la pamoja kutegemeana na hali ya bidhaa za maeneo husika zinazosafirishwa nje kupitia bandari zetu.

Bw. Mukasa ameongeza kuwa kupitia mikutano hii TASAC inatarajia kupata mafanikio ya kimaendeleo.

"Matarajio yetu kufuatia mkutano huu ni kuelewa vema mahitaji mahsusi na changamoto za usafirishaji wa Nyanda za Juu kusini ili kukuza uchumi wa nchi yetu, kuwawezesha wasafirishaji wa ukanda huu uelewa bora wa namna ya kutekeleza majukumu yao lakini pia kutuunganisha sisi wadhibiti na wadau wa usafirishaji katika ukanda wa bahari na maziwa." Alisema Bw. Mukasa.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa usafirishaji kutoka Mkoa wa Njombe, Ruvuma na Iringa, baadhi ya taasisi za serikali na sekta binafsi pamoja na kamati ya ulinzi na usalama mkoani Njombe.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo