Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

PROF. MBARAWA APONGEZA MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 09 February, 2026
PROF. MBARAWA APONGEZA MABORESHO BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amepongeza maboresho na uwekezaji unaofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam hali inayochochea kuongezeka shehena inayopitishwa katika bandari hiyo.

Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo tarehe 9 Februari, 2026 wakati alipofanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na kukagua uwekezaji na maboresho yanayofanywa katika kukabiliana na ongezeko la shehena bandarini hapo. 

Waziri Mbarawa amesema kuwa maboresho hayo yameongeza uwezo wa bandari kupokea na kuhudumia idadi  ya makontena, hatua ambayo inaongeza ufanisi wa bandari na kuimarisha mchango wake katika kukuza biashara na uchumi wa taifa.

Ameongeza kuwa uwekezaji uliofanywa na Kampuni za DP World  Dar es Salaam na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited, katika Bandari ya Dar es Salaam umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa shughuli za upakiaji na ushushaji wa makontena ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.


“Kabla ya maboresho hayo, shughuli za kupakia na kushusha makontena zilikuwa zikichukua muda mrefu, jambo lililosababisha msongamano na ucheleweshaji wa mizigo. Hata hivyo, kwa sasa mifumo ya kisasa na uendeshaji ulioboreshwa umewezesha makontena kushughulikiwa kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” ameeleza Waziri Mbarawa.

Waziri Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya uchukuzi ili kuhakikisha Bandari ya Dar es Salaam inaendelea kuwa lango kuu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani.

Katika ziara hiyo, Waziri Mbarawa amepata fursa ya kutembelea ujenzi wa mradi mkubwa wa  “Kurasini Logistic Park" unaotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), mradi huu ukikamilika utakua na uwezo wa kuhudumia makontena zaidi ya 700,000 kwa mwaka hivyo, kutatua changamoto za uondoshaji na uhifadhi wa makontena kwani maeneo mengi ya bandari kavu yamefikia kiwango cha juu cha uhifadhi kwa sasa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo