PROF. MBARAWA AFUNGUA MKUTANO WA 17 WA TATHMINI YA UTENDAJI WA SEKTA YA UCHUKUZI (JOINT TRANSPORT SECTOR REVIEW MEETING - JSTR)

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amefungua Mkutano wa 17 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (Joint Transport Sector Review Meeting- JSTR) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Prof. Mbarawa amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa Sera ya Taifa ya Usafiri Majini (National Maritime Policy).
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu nchi nzima ikiwemo ujenzi wa barabara za mwendo kasi jijini Dar es Salaam na ujenzi wa vipande vya SGR
Mhe. Prof. Mbarawa ameongeza kuwa kwa sasa Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza idadi ya safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kufikia sita (6) kwa siku.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linashiriki katika Mkutano huo wa siku tatu ulioanzq leo tarehe 23 Oktoba, 2024 na kufikia kilele tarehe 25 Oktoba, 2024 umeambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi zilizo chini ya Sekta ya Uchukuzi.
Mhe. Prof. Mbarawa alipata fursa ya kutembelea Banda la TASAC na kupata maelezo ya kina kuhusu majukumu ya Shirika hilo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Bw. Mohamed Salum.
Aidha Bw. Salum amesema pamoja na majukumu yanayotekelezwa na Shirika, lipo katika mkakati wa kubadilisha muundo na majukumu ya Shirika ili kuwa Mamlaka kamili ya udhibiti wa usafiri majini na kujikita katika majukumu ya kiudhibiti na kiutawala, (Maritime Regulation and Administration).
TASAC inashiriki Mkutano huo ikiwa ni mdau wa sekta ya uchukuzi, pamoja na kutumia maonesho yanayoendelea lengo la kujenga uelewa na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura 415 na mabadiliko yake.