PROF. KAHYARARA APONGEZA TASAC KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kusaidia maendeleo ya sekta ya uchukuzi hasa katika eneo la usafiri majini ikiwemo kusaidia kupungua kwa foleni ya meli za mizigo zinazoingia nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam
Prof. Kahyarara ameyasema hayo wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa TASAC, leo tarehe 01 Novemba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, mjini Kibaha, mkoani Pwani.
Akizungumza katika mkutano Prof. Kahyarara amesema kuwa TASAC imeshiriki katika kusimamia na kudhibiti bandari hivyo kusaidia kupungua kwa foleni ya meli zinazoingia bandarini hapa nchini.
"Hapo nyuma palikuwa na foleni ya meli zinazoingia nchini ila kwa sasa foleni imepungua, kutokana na michango ya utendaji wa wadau mbalimbali ikiwemo TASAC.
Prof. Kahyarara amewasihi watumishi wa TASAC kutumia fursa ya mkutano huo kutoa maoni, kujadiliana na kujenga mahusiano mazuri ili kuboresha utendaji wa Shirika.