Naibu Katibu Mkuu Uchukuzi atilia mkazo kuimarisha michezo
Dkt. Ally Possi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi ametoa maelekezo kwa Wakuu wa Idara za Rasilimali watu na Utawala wa taasisi zote za Wizara hiyo kuhakikisha wanaendeleza michezo sambamba na kuongeza ushiriki wa wafanyakazi katika michezo ili timu ya Uchukuzi iendelee kushinda katika mashindano mbalimbali ya baadae na kunufaika na faida za michezo kwa afya za wafanyakazi kama inavyoelekezwa na Serikali.
Ameyasema hayo jana tarehe 27 Julai, 2024 jijini Dodoma katika Ufunguzi wa Bonanza Maalum la Wizara ya Uchukuzi lililoandaliwa na Shirika la Reli Nchini (TRC) ikiwa ni sehemu ya hamasa ya ufunguzi wa huduma za Treni za umeme za Reli ya Kisasa (SGR) Dar es Salaam hadi Dodoma ambapo Mhe. Possi alikuwa mgeni Rasmi.
"Michezo ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, tuendeleze michezo ili tuimarishe afya zetu na kuongeza uwezo wetu wa kuchapa kazi. Bonanza linalofuata la Uchukuzi litafanyika jijini Mwanza na mwenyeji wetu atakuwa ni Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), ni muhimu tujipange mapema na mimi mwenyewe nitashiriki kucheza mchezo wa riadha." Amesema Dkt. Possi.
Aidha Dkt. Possi ametoa pongezi kwa TRC na Uongozi wa Klabu wa Uchukuzi kwa kuwezesha bonanza hilo lililoratibiwa vizuri na kuwezesha wafanyakazi waliojitokeza kwa wingi kushiriki michezo mbalimbali iliyoandaliwa ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba, michezo ya jadi, riadha na mingineyo.
‘'Natoa pongezi kwa wenzetu wa TRC na uongozi wa clabu ya uchukuzi na kamati nzima iliyowezesha bonanza hili, kiupekee nampongeza mwenyekiti wa klabu hii bw. Andrew Magombana, huyu ni mwanamichezo mzoefu na anayo historia nzuri ya kusimamia michezo." Amesema Dkt. Possi.
Katika bonanza hilo, Dkt. Possi alitoa medali na vikombe kwa washindi wa michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shirika la Uwakala wa Meli Nchini (TASAC) wamepokea kombe la mshindi wa kwanza na Kamba wanawake timu ya wizara ya Uchukuzi imepokea kombe la mshindi wa kwanza.