NAHODHA MANDIA ASISITIZA WELEDI KATIKA UTENDAJI KAZI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Naho. Mussa Mandia, leo tarehe 16 Juni 2025 amewashukuru Wajumbe wa bbodi pamoja na Menejimenti ya TASAC na kuwaasa kutekeleza majukumu waliyopangiwa kwa weledi ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa TASAC.
Naho. Mandia ameyasema hayo katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere Kibaha wakati wa Kikao cha Bodi wakati akikaribishwa tena na kupongezwa na Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya TASAC kwa kuteuliwa tena kuiongoza Bodi ya wakurugenzi kwa kipindi cha miaka minne.
“Napenda kuwashukuru sana kwa pongezi lakini naomba niwakumbushe kutekeleza majukumu yetu kwa weledi ili kutimiza majukumu ya TASAC,” amesema Naho. Mandia.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Bi. Rukia Shamte amempongeza Naho. Mussa H. Mandia kwa kuteuliwa tena na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania kuongoza Bodi hiyo ya Wakurugenzi kwa kipindi kingine cha miaka minne na kuiasa Menejimenti ya TASAC kuhakikisha inaendelea kushirikiana na Bodi kama ilivyokua katika kipindi chake cha kwanza.
Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya TASAC, Bw. Nahson Sigalla, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi amesema uteuzi huu ni heshima kubwa kwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo pamoja na Wakurugenzi wa Bodi hiyo na kuahidi kuwa Menejimenti ipo tayari kushirikiana na Bodi katika kuhakikisha kuwa Shirika linatekeleza majukumu yake.
Naho. Mandia ameteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 19 Mei, 2025 kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC kwa kipindi kingine cha miaka minne ikiwa ni mara ya pili kuteuliwa katika nafasi hiyo.