Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

NAHODHA MANDIA AFUNGUA MAFUNZO KWA BODI YA WAKURUGENZI

Imewekwa: 15 October, 2024
NAHODHA MANDIA AFUNGUA MAFUNZO KWA BODI YA WAKURUGENZI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, amefungua mafunzo Kuhusu Majukumu ya TASAC kwa wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha, mkoani Pwani.

Akifungua mafunzo hayo, Nah. Mandia amesema kuwa TASAC kama Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini, ina majukumu makubwa ya kusimamia na kudhibiti tasnia ya bahari nchini. 

“Jukumu letu sio tu kuhakikisha usalama, ulinzi, utunzaji mazingira ya bahari na maziwa na ufanisi katika shughuli za baharini ndani ya maji yetu lakini pia kuiunganisha Tanzania katika nyanda za kimataifa na kikanda,” amesema Nah. Mandia.

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha suala la usalama wa abiria na mali zao, TASAC iendelee kutekeleza mikakati yenye tija ya utoaji elimu kwa wadau wote muhimu ili utiifu wa Sheria za TASAC uwe endelevu.

“Naelekeza muendelee kutoa elimu ili utii wa sheria usionekane kuwa mzigo, bali kama sehemu muhimu ya kukuza tasnia ya bahari nchini na usafiri salama na utoaji huduma zenye ushindani” ameongeza Nah.Mandia.

Kwa upande, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema kuwa Shirika linatambua nafasi ya wadau hivyo, litaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wote wa Sekta Uchukuzi kwa njia  ili kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya usafiri wa majini vinakaguliwa mara kwa mara na vinakidhi vigezo vya kiusalama na kufuata masharti leseni ili kuhakiki usalama wa abiria pamoja mali zao. 

“TASAC tumetekeleza mpango Madhubuti wa ukaguzi wa vyombo majini na kupunguza ajali na kumarisha ufanisi wa huduma  za usafiri majini,” amesema Bw. Salum.

Aidha, ameongeza kuwa katika kuhakikisha usafiri endelevu wa majini, TASAC inaratibu na kusimamia Sheria zinazolenga  kulinda mazingira ya baharini, maziwa na mito. 

“Tunaendesha mazoezi ya utayari wa kusafisha mazingira hususan mafuta yakimwagika kutoka kwenye meli na vyombo vingine vya usafiri wa majini. Mpaka sasa hatuna tukio la umwagikaji mafuta katika eneo la maji ya Tanzania,” ameongeza Bw. Salum.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yanafanyika ili kuwajengea uelewa wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi kuhusu majukumu ya Shirika kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo