Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MWENYEKITI WA BODI TASAC AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA KATAVI

Imewekwa: 23 December, 2025
MWENYEKITI WA BODI TASAC AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MKOA WA KATAVI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, leo tarehe 22 Desemba 2025, amefanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, wakati wa ziara yake mkoani humo.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa kukagua maendeleo ya Bandari ya Karema pamoja na kushuhudia uzinduzi wa meli ya mizigo Jian Han 2 ya kampuni ya Nzenching International Company inayofanya shughuli zake katika Ziwa Tanganyika.

Nahodha Mandia ameeleza dhamira ya TASAC ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Mkoa wa Katavi ili kuhakikisha kuwa kanuni, sheria na miongozo ya usafiri wa majini vinazingatiwa, sambamba na kuboresha ubora wa huduma kwa maslahi ya watumiaji.

Kwa upande wake, Mhe. Mrindoko  ametumia mazungumzo hayo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuuwezesha Mkoa wa Katavi, kupitia ujenzi wa miundombinu muhimu, ikiwemo Bandari ya Karema iliyozinduliwa rasmi mwaka 2023.

Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umechochea kwa kiasi kikubwa, ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Katavi, kwa kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi na kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ndani ya muda mfupi.

Mhe. Mrindoko amesisitiza umuhimu wa sekta ya usafiri majini katika kukuza shughuli za kiuchumi, hususan biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo, na akaahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Mkoa na TASAC katika kutatua changamoto zilizopo.

Aidha, ameishukuru TASAC kwa kusimamia sekta ya usafiri majini, hususan katika maeneo ya usalama, ulinzi, mazingira, na udhibiti wa shughuli za usafiri majini.

Mazungumzo hayo yameweka msingi imara wa kuimarisha uratibu na ushirikiano kati ya TASAC na Serikali ya Mkoa wa Katavi, kwa lengo la kuhakikisha usafiri majini unakuwa salama, wa uhakika, na unaochangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Katavi na maeneo ya jirani.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo