Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Mwarobaini wa kuharakisha utoaji huduma bandarini watafutwa.

Imewekwa: 19 January, 2024
Mwarobaini wa kuharakisha utoaji huduma bandarini watafutwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Mohamedi Salum amekutana na Wasafirishaji Shehena Nje ya Nchi na Wapokeaji Shehena Ndani ya Nchi (Exporters and Importers) na kupokea maoni na changamoto wanazokutana nazo katika mnyororo wa  ugomboaji na uchukuzi kupitia bandari ya Dar es Salaam l tarehe 27 Desemba, 2023 jengo la SUMATRA jijini Dar es Salaam.

Wadau hao wameeleza baadhi ya changamoto ikiwemo mifumo isiyosomana miongoni mwa taasisi za serikali, mtandao katika ving’amuzi vinavyofungwa kwenye magari yanayobeba mizigo, ushirikiano hafifu miongoni mwa taasisi zinazofanya kazi katika kuchagisha mnyororo wa huduma za bandari na kutoweka kipaumbele kwa baadhi ya mizigo ambayo ni mali ghafi za viwandani na kusababisha uzalishaji viwandani kuchelewa au kufunga uzalishaji kutokana na kutopata malighafi kwa wakati au kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji viwandani. 

Bw. Mohamed Salum baada ya kupokea changamoto hizo akiwa kama mwenyekiti wa kikao hicho alimpa nafasi Mkurugenzi wa Huduma za Forodha wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Bw. Eustadius Mutatua kufafanua changamoto hizo.

 “Tumepokea changamoto hizo na tutakaa pamoja na taasisi zingine za serikali zinazofanya kazi bandarini na kujadiliana namna ya kila mmoja atakavyoondoa vikwazo na kuboresha mfumo wa mawasiliano ili kuharakisha mnyororo wa huduma." Bw. Mutatua.

 Aidha aliongeza kuwa TRA imeanzisha dawati linalofanya kazi masaa 24 kwa njia ya kupashana habari kwa WhatsApp na kuna Afisa anayeratibu mawasiliano kumplekea mhusika yeyote taarifa ya changamoto inayotokea.

Bw. Salum amehitimisha kwa kuwashukuru wadau hao na kusema mafanikio hayana kikomo kwa sababu watu wanaongezeka, uchumi unakuwa na mahitaji yanaongezeka . 
"Bandari zetu zinahitaji teknolojia, mtaji na wataalamu ili kuongeza ufanisi uendane sawa na mahitaji ya wateja wetu. hivyo kama mdhibiti tumepokea changamoto hizi na tutazichakata haraka na kuzishughulikia kwa kushirikiana na taasisi zingine za serikali kuzitatua na Wizara ya Uchukuzi." amesema Bw. Salum.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo