MLALI: TUMIENI WELEDI WENU KUPATA MAAFISA WAZURI MELINI

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Nelson Mlali ametoa wito kwa Bodi ya Mitihani ya Usaili wa Mabaharia kutumia nafasi walioipata, ujuzi na weledi wao kwa kusaili mabaharia wazuri ili kupata maafisa wa meli wabobezi watakaoweza kufanya kazi popote duniani.
Ameyasema hayo, leo tarehe 03 Machi, 2025 katika Makao Makuu ya Ofisi za TASAC zilizopo jijini Dar es salaam wakati wa ufunguzi rasmi wa mitihani ya kujieleza kwa ajili wahandishi na wataalam wa uendeshaji meli.
Amesema kuwa mabaharia wana mchango mkubwa katika kurahisisha shughuli za uchukuzi duniani kwa kuwa zaidi ya 80% ya biashara ya dunia inategemea usafiri wa maji hivyo, kupata mabaharia wenye sifa ni jambo la msingi katika kuongeza ufanisi katika minyororo ya usambazaji wa kimataifa.
"Ndugu wajumbe wa Bodi ya Mitihani ya Usaili nawaomba mtumie utaalam, ujuzi na maarifa mlionayo kufanya usaili wa maafisa melini ili kuwapata walio bora na mahiri wenye kukidhi vigezo vya mafunzo ya ubaharia kama inavyoelekezwa na Mikataba ya mafunzo ya Mabaharia duniani. Tunapokidhi vigezo vya Shirika la Bahari Duniani (IMO) vitasaidia mabahari hawa kuuzika katika masoko ya usafiri majini Kimataifa", amesema Bw. Mlali.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Udhibiti Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri na Utunzaji wa Mazingira Majini, Wakili Leticia Mutaki amewahimiza wanawake kusomea kozi za ubaharia na kufika ngazi za juu za ubaharia ili kuongeza idadi ya wahandisi na maafisa waongoza meli wa kike katika tasnia hii.
"Kwa sasa idadi ya wanawake katika tasnia ya ubaharia kwa ngazi ya maafisa ni ndogo sana. Naomba wanawake wajitokeze kwa wingi kusoma kozi katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), " amesema Wakili Mutaki.
Mitihani ya usaili wa maafisa waongoza meli na wahandisi wa meli itafanyika kuanzia leo tarehe 03 Machi, 2025 hadi 14 Machi, 2025.