Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Mkurugenzi Mkuu TASAC akizungumza kuhusu Utekelezaji wa majukumu ya TASAC na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24, jijini Dodoma.

Imewekwa: 28 July, 2023
Mkurugenzi Mkuu TASAC akizungumza kuhusu Utekelezaji  wa majukumu ya TASAC na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24, jijini Dodoma.

TASAC ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya Kifungu cha 4 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415 na kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe 23 Februari, 2018 baada ya Tangazo la Serikali Na. 53 kutolewa tarehe 16 Februari, 2018. 

Kuundwa kwa TASAC ni hatua ya kisera ya Serikali, kwa upande wa Tanzania Bara, inayokusudia kukuza sekta za usafiri majini, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuongeza mchango wa sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji. 

Nchi ya Tanzania ina ukanda mkubwa wa Bahari ya Hindi wenye urefu takriban Kilomita 1,424, Maziwa makubwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa; hivyo kuwepo kwa fursa kubwa ya kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia sekta hii, yaani uchumi wa rasilimali za maji (Blue Economy).

Aidha, TASAC inatekeleza majukumu matatu ambayo ni:

 i.Udhibiti wa huduma za usafiri majini. Katika kutekeleza hili jukumu, TASAC inafanya kazi zifuatazo za kutoa leseni, kusimamia viwango vya utendaji na kanuni za kusimamia Bandari, Bandari Kavu, watoa huduma ya Upimaji wa Uzito wa Makasha (Gross Mass Verification – GMV), Uwakala wa Meli (Shipping Agency), Uwakala wa Forodha (Clearing and Forwarding Agency), Ukusanyaji na Utawanyaji wa Shehena (Cargo Consolidation and De-consolidation), Udhibiti wa Watoa Huduma Mbalimbali Bandarini (Miscelaneous Port Services), Wahakiki shehena (Ship Tallying), pamoja na Wasafirishaji kwa njia ya maji (Shippers).

ii.Udhibiti wa  usalama na ulinzi wa usafiri majini na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za vyombo vya usafiri majini, majukumu ambayo hapo awali yalikuwa chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Kazi zinazofanywa ni kufanya kaguzi za vyombo vya usafiri majini, kutoa vyeti vya mabaharia, kutekeleza mikataba iliyoridhiwa na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania

iii.Kufanya huduma za biashara za meli kwenye eneo la Uwakala wa forodha. 
Kazi za Uwakala wa Forodha (Clearing & Forwarding Function) zinazofanywa katika bidhaa ambazo ni pamoja na; Kemikali zinazoagizwa ili kutumiwa kwenye migodi ya uchimbaji wa madini, sirahaza moto na vilipuzi, nyara za serikali, makinikia na Wanyama Pori kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa 
wanyama Pori Tanzania.


TASAC inatekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, majukumu makuu ya TASAC yapo kwenye vifungu vya 7, 11 na 12.

Katika kipindi Julai, 2022 hadi Juni, 2023; TASAC imeendelea kutekeleza kazi mbalimbali kama zilivyopangwa ili kutimiza malengo ya Mpango Mkakati wa Pili wa Shirika     wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) kama ifuatavyo:

TASAC imeendelea kuimarisha udhibiti huduma za usafiri majini, sambamba na kuhakikisha kuna ushindani sawia miongoni mwa watoa huduma kwa kutekeleza yafuatayo

Kuendelea kufanya ufuatiliaji, tathmini na kutoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa vigezo na viwango vya ubora wa huduma (performance standards and Benchmarks) kwa watoa huduma za bandari na usafiri majini; 

Kuratibu maombi ya tozo za usafiri wa meli katika Maziwa (Victoria na Nyasa) na kuhakikisha viwango vya tozo vinavyotumika haviathiri ushindani wa kibiashara;

Kuendelea na zoezi la urasimishaji wa bandari bubu Tanzania bara ambapo bandari bubu kumi na tatu (13) zilizowasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa ajili ya urasimishaji zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina kwa kushirikiana na TPA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo bandari bubu kumi zilionekana kukidhi vigezo hivyo na kupendekezwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) (WUU-U) kwa ajili ya kurasimishwa kwa mujibu wa sheria;

Aidha, waendeshaji wa zilizokuwa bandari bubu binafsi tano (05) za Mwanza ambazo ni miongoni mwa zilizokuwa bandari bubu ishirini (20) zilizorasimishwa kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 293/2022 wamepewa leseni za uendeshaji. TPA wameelekezwa kusimamia kwa karibu bandari kumi na tano (15) zilizobakia.

Kuboresha usalama, ulinzi wa vyombo vya usafiri majini na kudhibiti uchafuzi wa mazingira baharini na maziwa unaotoka kwenye meli. TASAC imeendelea kusimamia usalama, ulinzi wa vyombo     vya usafiri majini kwa; kufanya ukaguzi wa meli kubwa zibebazo zaidi ya tani 50 na vyombo vidogo vya majini ;

Shirika lilifanya kaguzi  ili kuhakikisha     kuwa ni salama na zinaendeshwa na mabaharia wenye sifa,uzoefu,utaalam na idadi inayostahili. Kazi hizo zimefanyika  katika mikoa ya Dar es Salaam,     , Tanga, Mtwara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Mbeya.Katika kipindi cha Julai, 2022     hadi Juni, 2023, Shirika lilifanya jumla ya kaguzi za meli kubwa 288 ambapo kaguzi 165     zilikuwa za meli za     kigeni na kaguzi 123 zilikuwa meli za ndani.  

#Aidha, TASAC imeratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji Majini kwa kutumia Kituo cha Utafutaji na Uokoaji Majini kilichopo Dar es Salaam (Maritime Rescue and Coordination Center – MRCC). Katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni, 2023; kituo kilipokea taarifa 4 za ajali zilizohusisha vyombo vya majini ambazo zilitokea katika eneo la maji ya Tanzania. Matukio ya ajali yalizoripotiwa katika Kituo cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji Majini. Katika ajali hizo jumla ya watu 61 walihusika ambapo watu 58 sawa na 95% waliokolewa na watu 3 sawa na 5% walipoteza maisha.

Utoaji wa Vyeti vya Mabaharia kwa Utaratibu wa Kimataifa (STCW-1978).TASAC imeendelea kutekeleza majukumu kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu     viwango vya Mafunzo ya Mabaharia (International Convention on Standards of Training,     Certification and Watch-keeping (STCW) for Seafarers 1978 as amended in 2010 (Manila     Amendment)) ili kuhakikisha kuwa vyombo vya usafiri majini vinaendeshwa na mabaharia     wenye sifa na uzoefu unaostahili. Jumla ya vyeti 16,546 vilitolewa na TASA kwa     mabaharia waliofuzu kwa kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni,2023 ambapo vyeti vya     Ustadi wa baharia (COP’s) vilikuwa 15,602,   vyeti vya utandaji wa baharia(CDC)vilikuwa     687 na vyeti vya umahiri wa mabaharia (COC) vyeti 257.

Kama mtakumbuka TASAC kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) na TAMISEMI ilifanya Sensa ya kwanza ya vyombo vidogo vya usafiri majini, ambapo     taarifa kuhusu vyombo, umiliki na mahali vilipo nchini zilikusanywa na kuingizwa katika kanzidata kwa malengo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha usimamizi wa usalama wa vyombo vya usafiri majini, utungaji wa sera na mipango itakayoongeza mchango wa uchumi wa rasilimali za maji (blue economy) katika pato la Taifa. Sensa hiyo imeonyesha takribani zaidi ya asilimia 53 ya vyombo hivyo viko ziwa Victoria, ikifuatiwa na bahari ya Hindi, ziwa Tanganyika na Nyasa.

Sensa ya namna hii ni     ya kwanza kufanyika nchini Tanzania na Afrika Mashariki. Kitabu cha Ripoti ya Sensa kilizinduliwa rasmi na Mhe. Naibu Waziri wa Nishati na Madini Bw. Atupele Mwakibete tarehe 11 Julai, 2023 na sasa kinapatikana katika tovuti ya Shirika.

Ili kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri majini na uvuvi, Serikali ya Awamu ya 6 kupitia TASAC inaendelea kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa kuboresha Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT ).

Lengo la Mradi huu ni kushughulikia changamoto za usafiri majini, kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria. Mradi huu unaotekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda umepangwa kugharimu kiasi cha Shilingi bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za Mradi ni Shilingi bilioni     19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani (national activities) na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda (regional activities) zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Disemba,     2024 na tayari Mkandarasi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi katika mradi huo. Hadi sasa, Mkandarasi ameshaanza ujenzi kwa vituo vidogo vya Mara-Musoma, Kanyala na Nansio-Ukerewe.

 *MPANGO MKAKATI WA UTEKELEZAJI KATIKA MWAKA WA FEDHA 2023/24* 

Katika bajeti ya mwaka 2023/24 TASAC imepqnga kuendelea kutekeleza yafuatayo:

Kuboresha udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji nchini sambamba na kuweka mizania sawa ya ushindani ili kuhakikisha huduma za usafiri majini zinakuwa endelevu.

Kuimarisha Usalama na Ulinzi kwa usafiri kwa njia ya maji sambamba na udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira utokanao na usafiri wa Meli.

Kuboresha usimamizi na uwajibikaji katika kupanga na kutumia rasilimali za Shirika

Kuimarisha uhusiano wa kitaasisi na kuongeza uelewa wa wadau kuhusu majukumu ya Shirika

Kuboresha Sheria, Kanuni, na nyenzo za kiudhibiti katika sekta za usafiri majini na biashara ya meli. 

Kutoa mafunzo kwa watumishi wake.

Katika kutekeleza hayo, TASAC itafanya yafuatayo:

Kuratibu maandalizi ya awali ya kutoa maoni na kuwezesha uandaaji wa rasimu za Kanuni na nyenzo za utendaji zitoazo mwongozo kuhusu udhibiti huduma za usafiri majini, usalama na ulinzi kwa vyombo vya usafiri majini na uchafuzi baharini kutoka katika meli; 

Kusimamia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji kwa njia ya Maji inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization); na

Kushirikisha wadau katika kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria na Kanuni mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, sura 415.

Napenda kuchukua nafasi hii kwa heshima kubwa kuishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha TASAC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa     Victoria (Multi-National Lake Victoria Maritime Communication and Transport- MLVMCT).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa alisema kuwa

"Serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha Bandari, ila mikataba na watakaoendesha shughuli hizo bado haijasainiwa.

Kwa sasa, wataalamu wako mezani kuzungumza kuhusu mikataba, muda na gharama.Wataalamu watakapokamilisha majadiliano tutaangalia maslahi yetu yako wapi na maoni yanayotolewa na Watanzania yatazingatia. Ndugu zangu hakuna bandari iliyouzwa kwa sababu Serikali iko macho wakati wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa.

*Imeandaliwa na TASAC.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo