Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MKURUGENZI MKUU TASAC ASAJILI PAPO KWA PAPO MABAHARIA WALIOKIDHI VIGEZO KATIKA KILELE CHA WIKI YA HUDUMA KWA MTEJA

Imewekwa: 13 October, 2025
MKURUGENZI MKUU TASAC ASAJILI PAPO KWA PAPO MABAHARIA WALIOKIDHI VIGEZO KATIKA KILELE CHA WIKI YA HUDUMA KWA MTEJA

Katika kuadhimisha kilele cha Wiki ya Huduma kwa Mteja, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amesajili papo kwa papo mabaharia waliokidhi vigezo katika zoezi lililofanyika katika Ofisi za Usajili za TASAC, zilizopo katika Jengo la PSSSF Garden Avenue Tower, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Salum alisema TASAC imeendesha usajili huo kama sehemu ya maadhimisho ya kimataifa ya Wiki ya Huduma kwa Mteja, mwaka huu ikiendeshwa kwa kaulimbiu “Mission: Possible”.

“Wiki hii inatukumbusha kwamba huduma bora kwa mteja inawezekana endapo tutajenga utamaduni wa kujituma, kushirikiana na kuwa wabunifu katika kazi zetu,” alisema Bw. Salum.

Bw. Salum pia alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa TASAC imejipanga kuanza kutoa vyeti vya kidigiti kwa mabaharia (digital seafarers’ certificates), hatua ya kisasa inayolenga kuboresha usimamizi, uhalisia na upatikanaji wa vyeti vya mabaharia kwa kutumia mifumo ya kidijiti.

“Kupitia mfumo huu, mabaharia wataweza kupata na kuthibitisha vyeti vyao kwa urahisi zaidi popote walipo. Vyeti vitakuwa na alama za usalama za kimataifa kama QR code na sahihi za kielektroniki ili kuondoa kabisa uwezekano wa kughushi,” alifafanua Bw. Salum.

Kwa upande wao, mabaharia walioshiriki katika zoezi hilo waliishukuru TASAC kwa jitihada zake katika kusimamia na kuboresha huduma ndani ya tasnia ya ubaharia nchini, wakisema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wateja kwa ukaribu.

Wakati huo huo, Bw. Salum alibainisha kuwa TASAC ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuhakikisha vyeti vya mabaharia vinavyotolewa nchini vinatambulika rasmi na Umoja wa Ulaya (EU).

“Kukubalika kwa vyeti vya Tanzania na Umoja wa Ulaya kutamaanisha mabaharia wetu wataweza kuajiriwa kwenye meli zinazomilikiwa na kampuni za Ulaya bila vikwazo vya kisheria,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa TASAC, juhudi hizo ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali ya Tanzania wa kuimarisha sekta ya usafiri majini kupitia matumizi ya TEHAMA.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo