Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA) Bi. Mtumwa Said Sandal asisitiza usafi wa fukwe uwe ni endelevu kwa wavuvi na wananchi waliopembezoni mwa bahari.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA) Bi. Mtumwa Said Sandal amesisitiza kuwa usafi wa fukwe uwe ni endelevu kwa wavuvi na wananchi waliopembezoni mwa bahari.
Ameyazungumza hayo katika zoezi la utoaji elimu ya Usalama wa Usafiri na Mazingira Majini pamoja na kufanya usafi katika ufukwe wa Kaole na Dunda katika kuelekea Kilele cha Siku ya Mabaharia Duniani leo tarehe 23 Juni, 2024.
"Muda mwingi wa maisha yenu mnashinda kwenye fukwe, usafi inabidi uwe endelevu kwa kulinda mazingira ya bahari kwa manufaa yetu sote na Taifa kwa ujumla." Amesema Bi. Mtumwa.
Naye Nahodha Ghadaf Chambo Afisa Mwandamizi Ukaguzi wa Meli TASAC amesema wavuvi wajenge tabia ya kuwa na vifaa okozi na kuvitumia pale wanapofanya shughuli mbalimbali za usafirishaji katika bahari, hiyo itasaidia kulinda maisha na nguvu ya inayotumika katika kuendeleza uvuvi na usafirishaji.
Aidha, Wavuvi Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani wameishukuru Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, TASAC na ZMA pamoja na wadau wa Usafiri Majini kwa kufanya Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani wilayani humo kwani kumewajengea uwezo wa kukabiliana na majanga yanayotokea majini.
Wadau wa Usafiri Majini wametoa vifaa vya usafiri kwa Halmashauri ya Bagamoyo Mkoani Pwani ili kuwezesha zoezi la usafi liwe endelevu katika maeneo ya fukwe.