MHESHIMIWA RAIS: UWEKEZAJI BANDARI YA TANGA KULETA AJIRA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji wa maboresho ya Bandari ya Tanga ambayo yamegharimu shilingi bilioni 429 utasaidia serikali kupata fedha zaidi zitakazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuleta ajira kwa wakazi wa Tanga.
Ameyasema hayo jijini Tanga, leo Machi 01, 2025 wakati alipokagua maboresho ya mradi wa gati mbili mpya katika Bandari ya Tanga na kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo.
Ameongeza kuwa maboresho hayo yatakwenda kuongeza ufanisi mkubwa wa bandari hiyo pamoja na kuliongezea tija taifa ambapo mpaka sasa maboresho hayo yamewezesha bandari hiyo kuhudumia tani milioni 1.2 ikiwa ni ongezeko ya zaidi ya tani laki saba (7) ukilinganisha na mwaka 2019/20 pamoja na kuongeza ajira kutoka 6000 hadi 17,000.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema wizara kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ipo mbioni kukamilisha mradi wa ununuzi wa boti mbili za utafutaji, uokozi na ukaguzi baharini wenye thamani ya bilioni 2.62.
Katika ziara hiyo TASAC iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Mohamed Salum.