Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MELI KUBWA MPYA YA KISASA YAWASILI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 22 September, 2025
MELI KUBWA MPYA YA KISASA YAWASILI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Meli ya Grande Shanghai kutoka nchini China imetia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam usiku wa tarehe 20 Septemba, 2025.
 
Meli hiyo maalum kwa ajili ya kubeba magari, ni mpya kabisa ambayo imetengenezwa mwaka 2025 inatumia nguvu ya umeme jua (solar power) ambayo ni teknolojia rafiki kwa mazingira badala ya kutumia mafuta katika uendeshaji wake.

Meli hiyo ya ghorofa 14 na urefu wa mita 220 ina uwezo wa kubeba magari 9,000 kwa  wakati mmoja. Kwa sasa meli hiyo inaendelea na ushushaji wa magari 1624 katika Bandari ya Dar es Salaam.
 
Wakizungumza wakati wa hafla fupi ya upokeaji wa meli hiyo, kwa niaba ya menejimenti ya meli hiyo, Bw. Girolamo Carignani amesema: “huu ni mwanzo kwa meli zetu kufika katika Bandari ya Dar es Salaam nchini Tanzania."

Amesema kuwa wataendelea kufanya safari za kuja nchini Tanzania ili kuboresha biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine, na kuongeza kuwa hivi karibuni itaanza safari za kwenda Japan kutokea China na kuja Tanzania.
 
Kwa upande wao wadau wa usafiri kwa njia ya maji wamefurahishwa na ujio wa meli ya hiyo na kusema kuwa imetatua changamoto kubwa ya wasafirishaji wa mzigo aina ya magari kwa kuwa meli nyingi huchanganya na mizigo mingine na magari.

Wadau hao wameishukuru Serikali kwa maboresho ya miundombinu na mifumo ya huduma za usafirishaji kwa njia ya maji.
 
Ujio wa meli kubwa nchini Tanzania haswa katika Bandari ya Dar es Salaam ni matokeo chanya ya upanuzi na maboresho katika bandari zetu nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo