Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MABAHARIA WATAKIWA KUWA MSTARI WA MBELE  KUSIMAMIA SHERIA ZA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 22 October, 2025
MABAHARIA WATAKIWA KUWA MSTARI WA MBELE  KUSIMAMIA SHERIA ZA USAFIRI MAJINI

Mabahari nchini wametakiwa kusimamia sheria na kuzingatia vihatarishi vinavyobainishwa na wataalam wakati wa kaguzi za ndani na kimataifa.

Wito huo umetolewa jana tarehe 21 Oktoba, 2025 na Kaimu Meneja Mafunzo na Utoaji Vyeti vya  Mabaharia wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mha. Lameck Sondo wakati wa Kikao Kazi cha Kurugenzi ya Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri Majini na Utunzaji wa Mazingira Majini (DMSE), kinachofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere mjini Kibaha. 


Mha. Sondo amesema kuwa wakati ni sasa kwa wakaguzi wa ndani ya meli kukutana pamoja na kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto za ukaguzi na kusisitiza katika kusimamia sheria za kitaifa na kimataifa.

"Muda umefika kwa wakaguzi wa ndani wa meli kukutana mara kwa mara na kujadiliana namna bora ya kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika ukaguzi, huku wakizingatia sheria za kitaifa na zile za kimataifa,” amesema Mha. Sondo.

Katika kikao hicho, watumishi wa DMSE wamepata fursa ya kusikiliza na kujadili mada mbalimbali kuhusu sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa, hoja zilizobainika katika ukaguzi uliopita, pamoja na vihatarishi vinavyoweza kuathiri utendaji kazi wa idara hiyo nyeti.

Kikao kazi hicho kinaendelea kwa lengo la kuboresha utendaji kazi, kuimarisha usalama baharini, na kuhakikisha mazingira ya kazi kwa mabaharia na wakaguzi yanazingatia viwango vya kimataifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo