Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

KONGAMANO LA BIASHARA NA USAFIRISHAJI TANZANIA LAZINDULIWA DUBAI

Imewekwa: 23 February, 2026
KONGAMANO LA BIASHARA NA USAFIRISHAJI TANZANIA LAZINDULIWA DUBAI

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, leo tarehe 13 Februari, 2026 amezindua Kongamano la Biashara na Usafirishaji Tanzania (Tanzania Trade & Logistics Forum) linalofanyika katika Hoteli ya Shangri-La, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Kongamano hilo linalenga kuimarisha uhusiano wa biashara na usafirishaji kati ya Tanzania na masoko ya kimataifa, kwa kuzingatia ukuaji wa fursa za kiuchumi barani Afrika.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo, Mhe. Londo amesema Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuvutia wafanyabiashara, hususan kutoka mataifa yasiyo na bahari, wanaopitisha mizigo yao kupitia bandari hiyo ikiwemo mizigo inayotoka UAE. 

“Bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bahari. Tunao wajibu wa kuendelea kuiboresha ili iwe na ushindani, iwe rahisi kutumia, na iwe chachu ya ukuaji wa uchumi wetu na wa ukanda,” amesema Mhe. Londo.

Ameongeza kuwa kongamano hilo ni fursa ya kuiunganisha Tanzania na masoko ya kimataifa, hususan Mashariki ya Kati, kwa kujenga mahusiano ya kibiashara yanayozingatia ufanisi wa usafirishaji, na uwekezaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasafirishaji wa Mizigo na Wamiliki wa Mizigo Tanzania uliopo Dubai (TANFORD), Bw. Hussein Jamal, amesema Wasafirishaji wa Mizigo kutoka Dubai wameamua kuandaa kongamano hilo ili kuonesha fursa zilizopo Tanzania na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuvutia wawekezaji wa nje.

“Tumeandaa kongamano hili ili kuonesha uzuri wa Tanzania na fursa zake za uwekezaji, na pia kuwaunganisha wadau wa usafirishaji na wamiliki wa mizigo na Serikali ili tuongeze biashara na uwekezaji unaopita kupitia Tanzania,” amesema Bw. Jamal.


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kongamano hilo, likiwa ni jukwaa muhimu la kujenga ushirikiano na wadau wa usafirishaji na biashara, pamoja na kuhamasisha mazingira salama, yenye ufanisi na yanayofuata taratibu katika shughuli za usafiri wa majini na huduma za bandari.

Kongamano hilo limeanza leo na linatarajiwa kufikia kilele kesho, tarehe 14 Februari, 2026.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo