KIKAO CHA IDARA YA HUDUMA ZA SHIRIKA (DCS) CHAFUNGULIWA RASMI MKOANI MOROGORO
Kikao cha Kurugenzi ya Huduma za Shirika (DCS) ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kimefanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 21 hadi 22 Novemba, 2025 mkoani Morogoro, kikihudhuriwa na watumishi 103 kutoka Sehemu za Rasilimaliwatu na Utawala, Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, pamoja na Masoko na Uhusiano.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu, Bw. Hamid Mbegu, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, alipongeza maandalizi na kusisitiza umuhimu wa kikao hiko katika kuboresha utendaji, kuimarisha mipango, na kujenga utamaduni chanya ndani ya Shirika.
“Kikao hiki muhimu kimelenga kufanya tathmini ya utendaji wa Idara, kujadili mipango na bajeti ya mwaka 2025/2026, pamoja na kupitia mwelekeo wa Shirika kutokana na Maendeleo ya mabadiliko ya Hadhi kutoka hadhi ya Shirika kwenda kuwa Mamlaka,” alisema Bw. Mbegu.
Katika hotuba yake, Bw. Mbegu alieleza kuwa mada zilizojadiliwa zinahusisha Maandalizi ya Mpango Mkakati wa Shirika, muundo wa shirika na mabadiliko yake ya hadhi, uimarishaji wa utamaduni wa taasisi (organization culture), pamoja na mikakati ya kujenga umoja na ushirikiano kazini (team building). Alisisitiza kuwa vikao vya aina hii vinaongeza uwazi, kuboresha mawasiliano, na kuchochea tija katika maeneo ya kazi.
Aliongeza kuwa kupitia majadiliano ya wazi, watumishi wanapata fursa ya kuainisha changamoto, kuibua mawazo mapya, na kuweka mikakati ya pamoja itakayowezesha Shirika kusonga mbele kwa ufanisi na weledi.
Bw. Mbegu aliwashukuru waandaaji, watoa mada, na washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi, na aliwahimiza kutumia kikao hiko kama chachu ya kuboresha utendaji wa kila siku na kuongeza thamani katika utoaji huduma.