Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

KATIBU MKUU UCHUKUZI AKAGUA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI MIZIGO KUTOKA BANDARI YA DAR ES SALAAM HADI BAHI

Imewekwa: 19 May, 2026
KATIBU MKUU UCHUKUZI AKAGUA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI MIZIGO KUTOKA BANDARI YA DAR ES SALAAM HADI BAHI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, leo tarehe 18 Mei, 2026 ameongoza viongozi na wadau mbalimbali katika ziara ya siku moja ya ukaguzi wa miundombinu ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia Morogoro hadi Bahi mkoani Dodoma, kwa lengo la kujionea utayari wa mifumo ya usafirishaji wa mizigo kwa kutumia reli ya kisasa ya SGR pamoja na reli ya MGR.

Ziara hiyo imehusisha viongozi kutoka taasisi mbalimbali za sekta ya uchukuzi, wakiwemo Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) pamoja na wadau wengine wa huduma za usafirishaji na biashara.

Lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kupunguza msongamano wa makontena bandarini, kupunguza foleni za malori barabarani na kuongeza matumizi ya reli katika usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Kahyarara amesema Serikali imejipanga kuhakikisha usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli unaimarishwa ili kuongeza tija katika Bandari ya Dar es Salaam na sekta ya uchukuzi kwa ujumla.

“Sisi kama Serikali mikakati yetu mikubwa ni kuhakikisha tunapambana na msongamano wa makontena uliopo bandarini, kupunguza foleni pamoja na kuongeza tija. Kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali, changamoto hizi zinaweza kuondoka kabisa,” alisema Prof. Kahyarara.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Machibya Masanja, amesema eneo la Bahi lina umuhimu mkubwa kimkakati katika kuimarisha usafirishaji wa mizigo nchini kupitia matumizi ya reli.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Julius Mitinje aliipongeza TRC kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa na kusisitiza kuwa TASAC ipo tayari kushirikiana na TRC pamoja na wadau wengine ili kuwezesha kuanza kwa mradi huo kwa wakati na kuongeza ufanisi katika mnyororo wa usafirishaji wa mizigo nchini.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha sekta ya uchukuzi, biashara na huduma za usafirishaji wa mizigo nchini kupitia matumizi ya miundombinu ya reli ya kisasa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo