Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) AIPONGEZA TASAC KWA KUIMARISHA HIFADHI YA MAZINGIRA YA USAFIRI MAJINI

Imewekwa: 13 July, 2026
KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) AIPONGEZA TASAC KWA KUIMARISHA HIFADHI YA MAZINGIRA YA USAFIRI MAJINI

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, tarehe 11 Julai, 2026 alitembelea Banda la Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA), ambapo alipongeza jitihada za shirika hilo katika kusimamia usalama wa usafiri majini na kulinda mazingira ya bahari, maziwa na mito nchini.

 

Akipokea maelezo ya shughuli za TASAC, Dkt. Muyungi amesema usimamizi madhubuti wa mazingira ya usafiri majini ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu na uchumi wa buluu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatia sheria na viwango vya kitaifa na kimataifa vya uhifadhi wa mazingira.

 

"Serikali inaendelea kuweka mkazo katika uhifadhi wa mazingira kupitia utekelezaji wa sheria, matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa taasisi mbalimbali. TASAC ina nafasi muhimu katika kuhakikisha shughuli zote za usafiri majini zinafanyika kwa kuzingatia usalama na kulinda mazingira," amesema Dkt. Muyungi.

 

Akiwa katika bandani hapo, Dkt. Muyungi alipatiwa maelezo kuhusu majukumu ya Shirika katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya usafiri majini.

 

Alielezwa kuwa TASAC linasimamia utekelezaji wa sheria na mikataba ya kimataifa inayohusu kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na meli, kufanya ukaguzi wa vyombo vya majini ili kuhakikisha vinazingatia viwango vya mazingira, pamoja na kuratibu maandalizi na mwitikio wa matukio ya uchafuzi wa mafuta na kemikali katika bahari, maziwa na mito nchini.

 

Katika ziara hiyo, Dkt. Muyungi alipata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali za banda la TASAC na kujionea huduma zinazotolewa na shirika, ikiwemo usimamizi wa usalama wa usafiri majini, utafutaji na uokoaji, usajili wa mabaharia, pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuzuia uchafuzi wa mazingira ya majini.

 

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma na binafsi zinazoonesha bidhaa, huduma na ubunifu unaochochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo