KANALI MTAMBI AELEZEA MIKAKATI YA SERIKALI SEKTA YA USAFIRI MAJINI
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amesema Serikali inaendelea kutekeleza Sera mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri katika nyanja zote ikiwemo wasafiri wanaotumia njia ya maji.
Kanali Mtambi ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Usafiri kwa njia ya Maji Duniani yaliyofanyika tarehe 26 Septemba, 2024 katika viwanja Vya Mkendo, Mkoa wa Mara, Wilaya ya Musoma.
“Serikali imedhamiria kuhakikisha inaboresha sekta hii kwa kuwekeza katika miundombinu na vyombo vya usafiri majini, kuingia katika mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya kulinda mazingira ya bahari au maziwa na viumbe, ili kuhakikisha jamii inapata maendeleo endelevu." Amesema Kanali Mtambi.
Aidha, Kanali Mtambi ameongeza kuwa, katika kuhakikisha Serikali inatekeleza mikakati hiyo wananchi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanatumia kwa kuzingatia viwango stahiki vya Usalama.
“Tanzania ina eneo kubwa la maji ukilinganisha na nchi nyingi Barani Afrika, takribrani kilomita za mraba 223,000 ukiacha eneo la bahari yapo maziwa makuu kama Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa yenye ukubwa wa kilometa za mraba 64,5000. Maeneo yote haya ya maji ni muhimu sana kwa uchumi wetu kama yatatumiwa kwa kuzingatiwa viwango stahiki vya usafiri salama kwa taratibu stahii na kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira na rasilimali zilizopo basi yatakuwa na faida kubwa na endelevu kwa jamii yetu.” Ameongeza Kanali Mtambi.
Pia, Kanali Mtambi amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo pamoja na kamati ya maandalizi kwa kuchagua Mkoa wa Mara kwa kuwa eneo kubwa la Mkoa huo linazungukwa na Ziwa.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza sana wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli mbalimbali katika maoenesho haya siku kwa siku. Ninaamini kuwa tumepata elimu nzuri ya usalama wa vyombo vya usafiri katika maji, usalama katika mialo, usalama katika visiwa vyetu." Amesema Kanali Mtambi.