KAMISHNA MKUU TRA AKUTANA NA MKURUGENZI MKUU TASAC KUJADILI UBORESHAJI WA SEKTA YA USAFIRI WA MAJINI
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Mwenda, leo tarehe 8 Desemba, 2025, amemwalika na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na huduma zinazodhibitiwa na TASAC.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha uratibu wa taasisi zake katika kuendeleza na kuboresha sekta ya usafiri wa majini.
Majadiliano yamelenga kuimarisha ushirikiano wa kikazi kati ya TASAC na TRA, kurahisisha taratibu za kikodi, pamoja na masuala ya ushuru na forodha yanayohusu shughuli za bandari kwa waendeshaji wa huduma za usafiri wa majini, pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na utozaji wa kodi za forodha bila kuathiri ukuaji wa sekta.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mwenda amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kuboresha mifumo ya forodha, sambamba na kukuza sekta ya usafiri wa majini kwa manufaa ya uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Bw. Salum ameeleza dhamira ya TASAC ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na TRA ili kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini inasimamiwa kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya kimataifa, huku masuala ya ushuru na forodha yakisimamiwa kwa uwazi na weledi.
Aidha, pande hizo mbili zimejadiliana changamoto za kiutendaji katika shughuli za bandari, meli, ushuru wa forodha na usafiri wa ndani ya maji pamoja na namna bora ya kuzitatua kwa kushirikiana.
Pande zote mbili zimekubaliana kuwa ushirikiano wa karibu kati ya TASAC na TRA ni wa msingi katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini inakuwa na mifumo imara ya usimamizi, ukusanyaji wa mapato, ushuru na forodha inayotekelezwa kwa ufanisi, pamoja na mazingira rafiki ya biashara kwa wawekezaji na waendeshaji wa huduma za majini.