KAMATI YA KUDUMU YA BARAZA LA WAWAKILISHI MAWASILIANO, ARDHI NA NISHATI ZANZIBAR, YAIPONGEZA TASAC

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa bandari na bandari kavu hapa nchini pamoja na usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira wa usafiri majini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, leo tarehe 03 Februari 2025, walipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na kupongeza utendaji kazi katika Bandari hiyo na kupata matokeo chanya yenye maslahi mapana kwa Taifa.
“Tumefurahishwa na utendaji kazi mzuri wa TASAC katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari hii ya Tanga ambayo kwa kiasi kikubwa imerahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani kwa eneo hili la mwambao ambalo lilikua na changamoto kubwa ya usafiri kwa njia ya maji,” amesema Mhe. Abdulla.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti Mha. Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na mashirikiano katika kudhibiti shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mha. Sondo ameongeza kuwa TASAC inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria ambao ni mradi wa ushirikishwaji wa nchi za Uganda na Tanzania katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia TASAC imeendelea na ujenzi wa kituo kikuu cha uratibu wa masuala ya Utafutaji na Uokozi (MRCC) katika Ziwa Victoria.
Aidha, ameelezea kufanikiwa kwa hali ya juu katika ukaguzi wa meli za kigeni, pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ya kuwajengea uwezo watumishi wake katika kutekeleza majukumu hayo ya kiudhibiti.
Kamati hiyo inafanya ziara hiyo kuanzia tarehe 03- 04 Februari, 2025 lengo la kujifunza utendaji kazi pamoja na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAC na TPA mkoani Tanga ikiwemo Bandari za Tanga, Pangani na Kipumbwi.