Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

DK. BITEKO AZITAKA MAMLAKA ZA USAFIRISHAJI MAJINI BARANI AFRIKA KUSHIRIKIANA

Imewekwa: 29 November, 2024
DK. BITEKO AZITAKA MAMLAKA ZA USAFIRISHAJI MAJINI BARANI AFRIKA KUSHIRIKIANA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, leo, tarehe Novemba 29, 2024 amezitaka Jumuiya ya Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri majini Barani Afrika (AAMA) kushirikiana na kuungana ili kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji majini na hivyo kuchochea maendeleo ya Uchumi katika nchi husika.

Dkt. Biteko ametoa ushauri huo wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Saba wa AAMA unaofanyika kwa siku tatu, Jijini Dar es Salaam.

“Kila mmoja wetu atumie fursa ya mkutano huu kujiwekea malengo yatakayo tuwezesha kufikia azma ya kuboresha usalama na kuimarisha sekta ya usafirishaji wa majini” amesema Dkt. Biteko.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema miongoni masuala yanayohitaji kutiliwa mkazo ni pamoja na suala la rasilimali watu hususan vijana ambao watachagiza maendeleo na ukuaji wa sekta ya usafiri na usalama wa usafirishaji wa majini.

Prof. Mbarawa amesema Tanzazania kwa upande wake imekuwa mstari wa mbele ikitekeleza maazimio ya uboreshaji wa sekta hiyo ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa inayolenga pamoja na mambo mengine, kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Masuala ya Baharini (IMO), Arsenio Dominguez ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Kongamano na Mkutano huo suala linaloonesha utayari wake katika uboreshaji wa sekta ya usafirishaji na usalama wa majini.

Dominguez amesema  IMO itaendelea kuwezesha vikao hivyo vya kimataifa ili kujenga na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama ili kukabiliana na changamoto katika nchi husika.

Lengo la mkutano huu ni kujadili masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya uthibiti na usimamizi wa usafiri majini Barani Afrika, kipaumbele kikiwa ni kupata mustakabali wa usafiri majini pamoja na kuongeza ushirikiano baina ya nchi wanachama.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo